Siku ya nne ya kufungwa kwa shughuli za serikali ya Marekani
5 Oktoba 2013Huku wabunge wakiianza wikendi ya kwanza wakati ambapo bado shughuli za serikali zimefungwa na bunge kutoonekana kuutatua mkwamo huo, hii inatazamiwa kuleta athari zaidi huku Marekani ikionekana kuwa itashindwa kulipa madeni yake katika siku 12 zijazo iwapo hali hiyo itakuwa bado inaendelea.
"Huu sio mchezo," alisema spika wa bunge John Boehner, ambaye ni mmoja wa viongozi wa Republican katika bunge la Marekani, Congress.
Boehner alitamka maneno hayo baada ya gazeti moja la kila siku nchini humo kuandika ripoti na kumnukuu afisa mmoja mkuu serikalini ambaye hakutajwa jina akisema ikulu ya Marekani inafaidika kutokana na hali hiyo iliowalazimu maelfu ya wafanyakazi wa serikali kukaa nyumba bila malipo.
"Raia wa Marekani hawataki serikali yao ifungwe na mimi pia sipendi hilo, kile tunachotaka ni kuwa na majadiliano, kufungua tena shughuli za serikali na kuleta usawa miongoni mwa Wamarekani waliochini ya mpango wa afya wa Obamacare,'" Alisema John Boehner.
Obama azungumzia kufungwa kwa shughuli za serikali
"hakuna ushindi wowote utapatikana hapo ikiwa familia hazina uhakika wowote wa iwapo watalipwa mishahara yao au la," Alisema Obama. Hatua hii ya kufungwa kwa serikali ya Marekani imetokea baada ya miaka 17 ya tukio kama hilo nchini Marekani.
Shughuli za baadhi ya ofisi za serikali ya Marekani zilifungwa siku ya Jumanne kufuatia bunge la nchi hiyo kushindwa kufikia makubaliano juu ya bajeti mpya. Warepublikan ambao wanadhibiti sehemu kubwa ya baraza la wawakilishi wanataka kucheleweshwa kwa mpango wa rais Obama wa kutoa huduma ya afya ujulikanao kama Obamacare.
Wabunge hao wa Republican wanashinikiza sheria hiyo ya mabadiliko ya afya iondolewe au mpango huo hautapokea fedha za kuugharamia. Kwa sasa Obama amemuomba Spika Boehner kuitisha kura ya kuugharamia mpango wa afya wa Obama care kwa muda na kufungua shughuli za serikali.
Hata hivyo wabunge wa chama cha Democratic na wale wa Republikan kwa sasa hawaonekani kuwa katika njia moja ya kusuluhisha tofauti zao.
Obama kwa upande wake amekataa kuwa na mazungumzo ya aina yoyote na Warepublican hadi pale watakapofungua shughuli za serikali na kupitisha mswada utakaowezesha mpango wa obama care kugharamiwa kwa muda na kukubali kuongeza uwezo wa serikali kukopa kufikia kiwango cha dola trilioni 16.7. Na Warepublikana nao wanasisitiza kuwa Obama akubali kujadiliana nao na kukubali kucheleweshwa kwa sheria ya mabadiliko katika mpango wa Obamacare jambo ambalo rais amekataa kulitekeleza.
Ziara ya Obama barani Asia yafutiliwa mbali
Kwa wakati huu rais huyo wa Marekani anakabiliwa na hali ya fedheha namna watu wanavyoiangalia Marekani barani Ulaya na pia kupata pigo kwa sera zake za kigeni kwa kufuta ziara yake barani Asia na pia kutohudhuria mikutano miwili ya kimataifa kutokana na kufungwa kwa shughuli za serikali yake.
Siku ya Alhamisi wiki Hii Obama alichukua hatua ya kufuta ziara yake mjini Bali Indonesia alikokuwa anatarajiwa kuhudhuria mkutano wa Uchumi wa eneo la Asia Pasifik, na Brunei alikokuwa ahudhurie mkutano wa uchumi wa mataifa ya eneo la Mashariki mwa Asia.
Kwa sasa wachambuzi wanasema kwamba hili ni pigo kubwa katika sera yake ya kigeni ya kutaka maswala ya kidiplomasia na ya kijeshi kutiliwa maanani katika kuliinua bara hilo.
Mwandishi: Amina Abubakar/AFP
Mhariri: Sekione Kitojo