1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Siku ya 2 ya chaguzi za ndani za chama tawala Tanzania CCM

21 Julai 2020

Chama tawala nchini Tanzania CCM, leo kinakamilisha ungwe yake ya mwisho ya mchujo wa wagombea wa ubunge katika uchaguzi mkuu ujao huku vigogo kadhaa wakianguka vibaya.

Tansania Sansibar| Hussein Ali Mwinyi
Picha: DW/Said Khamis

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya habari vigogo kadhaa ikiwamo wabunge waliohamia chama hicho kutoka upinzani hivi karibuni wameanguka vibaya katika kura za maoni. Wanasiasa hao waliokuwa upinzani na baadaye kuvikacha vyama vyao na kujiunga na chama hicho tawala, sasa wanajikuta njia panda baada ya kufanya vibaya katika majimbo waliyowania huku wengine wakiondoka na kura chache.

Kuanzia majimbo ya mkoa wa Dar es Salaam ambako wabunge wake walikwenda CCM na kisha kurejeshwa tena kupitia chama hicho, mpaka majimbo ya hivi karibuni kabisa ambako wabunge wengine walijiengua na upinzani, kote huku vumbi limewatimkia wabunge hao. Kwenye kura hizo za maoni wengi wao wamejikuta wakishika nafasi za chini na ingawa baadhi yao wamekamata nafasi za katikati.

Hali mbaya kwa wengi miongoni mwa waliohamia CCM kwa kuunga mkono serikali

Aliyekuwa katibu mkuu wa CHADEMA Vincent Mashinji na Msemaji wa CCM Humphrey PolepolePicha: DW/Said Khamis

Hata hivyo, mbunge mmoja tu aliyejiunga na chama hicho tawala amefanikiwa kupenya kwenye kura hizo za maoni, mbunge wa jimbo la Siha ambaye pia ni naibu wa waziri wa afya aliyefanikiwa kushika nafasia ya kwanza. Kitendo hiko cha wabunge hao kufanya vibaya kwenye kura za maoni ni moja ya mada inayojadiliwa kwa kiwango kikubwa wakati huu. Sam Ruhuza ambaye kwa muda mrefu amekuwa akishiriki siasa za vyama vya upinzani, anasema kile walichokutana wabunge hao ni ujumbe tosha kwa wanasiasa wengine katika siku za usoni.

Mkuu wa mkowa wa Dar es Salaam ni miongoni mwa walioshindwa katika kura za maoni

Wagombea wengine ambao walikuwa viongozi serikali na kisha kuziacha nafasi zao na kwenda majimboni nao pia wameadhibiwa na wapigakura. Viongozi kama waliokuwa wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya pamoja na wakurugenzi wameshindwa kung'ara kwenye mchakato huo wa kura za maoni. Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda na waziri wa habari, utamaduni na michezo, Dk. Harrisojn Mwakyembe ni baadhi ya vigogo hao ambao kura hizi za maoni zimewaendea kombo kwao.

Waandishi wa habari waliojitosa kwenye kinyang'anyiro hicho pamoja na kundi kubwa la wasanii walikuwa na nia ya kwenda bungeni kupitia chama hicho, ni kundi lingine ambalo kura hizo za maoni hazikutosha kwao. Hata hivyo, baadhi ya mawaziri walioingia bungeni kwa kuteuliwa na Rais wamefanikiwa kupata uungwaji mkono katika majimbo yaliyojitosa kwa mara ya kwanza kwa kuongoza katika matokeo ya kura za maoni.

Soma zaidi:Uchaguzi Mkuu Tanzania Oktoba 28 

Chama hicho leo kinakamilisha ungwe yake ya mwisho ya kura za maoni huku macho ya wengi yakielekezwa katika jimbo la Kawe Jijini Dar es salaam ambako wagombea zaidi ya 100 wamekuwa wakichuana. Jimbo hilo limewavutia wanasiasa wakongwe, wale chipukizi, viongozi wa dini, wafanyabiashara na watu wengine wenye ushawishi katika jamii.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW