1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Siku ya Twakimu Afrika - Umuhimu wa takwimu Zanzibar

17 Novemba 2023

Wakati Afrika inaadhimisha siku yake ya Takwimu, suala la matumizi ya takwimu hizo kuleta maendeleo na kupambana na changamoto haijafikia katika kiwango kinachoridhika.

Nigeria | Mwanamke na mwanae
Mwanamke na mtoto wake Picha: Fati Abubakar/AFP/Getty Images

Zanzibar ni miongoni mwa nchi za Afrika ambapo kwa hivi karibuni imekuwa ikiyapa kipaumbele matumizi ya takwimu katika kupambana na udhalilishaji, suala ambalo limekuwa ni changamoto kwa maendeleo ya wanawake na watoto.


Ofisini ya mtakwimu mkuu Zanzibar imejiwekea utaratibu wa kila mwezi kuripoti matukio ya udhalilishaji ambapo kwa mwezi wa septemba mwaka huu wa 2023, jumla ya matukio 157 ya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia yaliripotiwa ambapo zaidi ya asilimia 70 wakiwa ni watoto waliobakwa. 

Matukio hayo yamekuwa yakibadilika kila mwezi kati ya matukio zaidi ya 70 kwa wastani, hali inaonesha kuwa udhalilishaji wa wanawake na watoto bado ni suala linalohitaji nguvu ya pamoja inayojumuisha jamii na vyombo vya sheria katika kukabiliana nalo. 

Tangu kuanza kwa matumizi ya takwimu kumeleta mabadiliko makubwa hasa katika kuzidisha harakati za kupinga udhalilishaji pamoja na kuweka mipango ya serikali ya kukabiliana na tatizo hilo ikiwa ni pamoja na uimarishaji wa sheria.

Watafiti wamekuwa wakielezea umuhimu wa kutumia takwimu ambazo huwaongoza katika muelekeo wa kupanga na mikakati ya utoaji wa elimu kwa jamii na kutatua tatizo kama anavyoeleza mtaalamu wa takwimu Zuwena Abdallah Hilal.

Serikali kwa kushirikiana na wadau wameamua kutoa takwimu za kila mwezi ili kuonesha hali halisi ya tatizo hilo lakini changamoto inayojitokeza ni ushirikiano mdogo kutoka kwa wananchi kusita kutoa taarifa.

Kauli mbiu ya mwaka huu ya maadhimisho ya takwimu yanahimiza matumizi ya takwimu katika kuimarisha ushirikiano katika nchi za Afrika hasa katika utatuzi wa changamoto mbali mbali. 


Kwa mujibu wa mashirika ya kimataifa ikiwemo UNICEF, UN Women na WHO yamekuwa yakitoa wito kwa nchi kuimarisha suala la ukusanyaji wa takwimu ikiwa ni njia moja wapo ya kuimarisha ulinzi kwa watoto na wanawake lakini suala hilo limekuwa na changamoto kutokana na uwezo wa kiuchumi ambapo nchi kadhaa bado zinategemea ufadhili kutoka nje.

Mwandishi: Salma Said DW Zanzibar