1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Siku ya wanawake ulimwenguni

7 Machi 2006

Eti juhudi za kuleta haki na usawa kati ya wanaume na wanaweka zimefikia wapi?

Wanawake bado wanadai haki ya kupiga kura nchini Kuweít
Wanawake bado wanadai haki ya kupiga kura nchini KuweítPicha: AP

Maendeleo ya wanawake ni maendeleo ya ulimwengu mzima-matamshi hayo yalitiliwa mkazo na viongozi wa taifa na serikali walipokutana katika hadhara kuu ya umoja wa mataifa mwaka jana mjini New-York.Hali halisi lakini ikoje?Katika hotuba yake ya mwaka huu kuadhimisha siku ya wakinamama ulimwenguni,katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Kofi Annan ametoa mwito kwa mara nyengine tena mataifa yahakikishe haki sawa kwa jinsia zote mbili.Na ili ahadi ziwe ukweli wa mambo panahitajika miradi madhubuti ya kuwaelimisha wakinamama kuweza kushiriki kikamilifu katika harakati za akisiasa na kiuchumi.

Tangu miezi michache iliyopita,Liberia,Ujerumani na Chile zinajikuta zinaongozwa na wanawake.Na hata kama mtu hawezi kulinganisha si mataifa hayo matatu na wala si viongozi hao waliochaguliwa,lakini matarajio ya walimwengu katika nchi zao ni ya aina moja.Wanatakiwa walete msukumo wa kisiasa kule ambako wenzao wa kiume wameshindwa kufdanya hivyo.Wanawekewa matumaini mema sawa na viongozi wenzao katika nchi nane nyengine za dunia.

Wanawake wanawakilishwa hivi sasa katika mabungu chungu nzima.Zaidi ya asili mia 16 ya viti vya bunge vinakaliwa na wakinamama-hali hiyo haijawahi kushuhudiwa hapo awali.Ndo kusema jamii ya mabwana inakurubia kumalizika?Ndo kusema ni suala la wakati tuu hadi mitindo ya kubaguliwa wakinamama itakapokoma?Na jee suala la kuwajibika wakinamama katika jamii isiyo ya kibaguzi limegeuka ukweli wa mambo?

Hasha.Asili mia 16 ni nini tukizingatia ukweli kwamba zaidi ya nusu ya wakaazi wa dunia ni wanawake?Kuwakilishwa wakinamama bungeni,si tukio kubwa hivyo tukitilia maanani kwamba katika kipindi cha miaka 30 iliyopita idadi ya wabunge wakike imeongezeka kwa asili mia tano tuu.Takwimu hizo hata hivyo zinaonyesha mambo yanasonga mbele,japo kama katika nchi nyingi bado idadi ya wakinamama wanaowakilishwa bungeni ni chini ya kile kiwango kilichowekwa cha asili mia 30.

Kiwango hicho kitakapofikiwa tuu ndipo tutakapoweza kuzungumzia juu ya azma ya kweli ya kuvunja duara ya wanaume wanaopendelea zaidi kugawana madaraka kuliko kuwajibika kijamii na kiutu kama vile ukweli wa maisha ya wakina mama unavyoonyesha.

Hata katika uchumi hakuna mengi yaliyobadilika.Bado ni wakinamama wachache wanaoajiriwa makazini wakilinganishwa na wenzao wa kiume.Na wanapopata kazi,mara nyingi hawana cheo wala ushawishi.Wanafanya kazi moja,lakini mwanamke analipwa haba kuliko mwenzake wa kiume.Na hata kama baadhi ya mashirika yamekua hivi sasa yakiwaachia wakinamama kushikilia nyadhifa za juu-kileleni-kule yanakopitishwa maamuzi ya madaraka na fedha,lakini bado wanaume wanaongoza.Nchini Ujerumani kwa mfano kiwango cha madhamana wa kike katika mashirika makubwa makubwa,ni asili mia nne tuu.

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Kofi Annan anapozungumzia juu ya umuhimu wa kuwepo haki sawa kati ya wanawake na wanaume,anafanya kile kila mtu anachokitarajia.Wakati kwa hivyo umewadia kwa serikali,mashirika na makampuni kupania na kufungua njia za kushirikishwa wakinamama katika daraja zote za maendeleo-kisiasa na kiuchumi.Ni muhimu kuliko wakati wowote mwengine kuwashirikisha wakinamama hasa katika wakati huu ambapo mizozo ya kisiasa na kiuchumi inapamba moto.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW