1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Siku ya Watakatifu

Annette Morczinek / Maja Dreyer31 Oktoba 2005

Tarehe moja Novemba waumini wa kanisa la katoliki duniani kote wanasherehekea siku ya watakatifu ambayo ni siku ya kwenda makaburini na kuwakumbuka wale waliokufa. Lakini nchini Ujerumani utamaduni wa mazishi pamoja na kupamba makaburi unabadilika.

Makaburini ya kawaida nchini Ujerumani
Makaburini ya kawaida nchini UjerumaniPicha: BilderBox

Kwa mujibu wa kura ya maoni, bado Wajerumani wengi wanataka mazishi yao yao ya kawaida kama ni kuchomwa na majivu yatiwe katika kombe kama bibi huyu anavyoomba: "Ndiyo, afadhali kuchoma maiti yangu kwa sababu ni rahisi zaidi kwa jamii yangu."

Wengine wanataka mazishi ya kawaida pamoja na jeneza, kama mwanamume huyu: "Nitakapokufa nataka mazishi ya kawaida, anasema huyu. Kwa kweli gharama ni kubwa zaidi na kweli pia, mimi sitahisi kitu kwa sababu nitakuwa nimeshakufa, lakini hata hivyo nisingependa maiti yangu ichomwe."

Mbali ya hao wawili, kila mwaka asilimia 15 ya watu 820.000 waliokufa nchini Ujerumani walipewa mazishi bila jina na idadi ya Wajerumani wanaotaka mazishi baharini au msituni.

Wanaweza kwa mfano kununua haki ya majivu yao kuzikwa karibu na mti katika misitu fulani inayotumika kwa ajili hiyo tu. Mazishi kama hayo yana bei ya Euro 800 ambayo ni rahisi ukilinganisha na bei za kawaida za mazishi ya makaburini ambayo yanagharamu Euro elfu mbili au tatu. Sababu nyingine ni muundo wa familia unabadilika au unavunjika.

Mtaalamu wa mambo ya saikolojia Silke Haase anaamini kwamba namna ya kuwaaga wale waliokufa inabadilika: "Kwa watu wengi, si muhimu kuwa na kaburi la mwenzake linaloweza kutembelewa, lakini wanatafuta njia nyingine ya kuendelea na mahusiano na marehemu."

Asilimia 40 ya Wajerumani wanataka mazishi bila jina, idadi ambayo inazidi kuongezeka. Makanisa ya katoliki na ya kilutheri yanalalamika kuhusu mwelekeo huo kwani unatokana na jambo lingine linalozusha wasi wasi yaani idadi ya wazee wanaokaa peke yao na wanaokufa peke yao inaongezeka. Mazishi bila jina yataimarisha mwelekeo huo, makanisa yanasisitiza. Badala yake mazishi ya kawaida huwakumbusha watu juu ya yule aliyekufa.

Pamoja na hilo, pakiwepo na mahala pa kumkumbuka mtu, kama vile jiwe linalowekwa juu ya kaburi likiwa na jina la marehemu huwasaidia watu wengi katika huzuni wao. Wengi waliofiwa ambao kwanza walikubali mazishi bila jina, baadaye hupata shida kwa kukosa kuwa na mahala pa kuomboleza.

Kampuni zinazotengeza majeneza na mashirika yanayosimamia mazishi wanajiambatanisha na mwelekeo huo kwa kubadilisha huduma zao. Kwa mfano waliofiwa wanaweza kuchagua musiki gani utumike kwenye mazishi au wenyewe wanaweza kutia rangi jeneza.

Makanisa lakini yanapinga mabadiliko haya ya utamaduni wa mazishi kama askofu Joachim Wanke anavyoeleza: "Zamani maslahi ya mtu aliyekufa yalipewa umuhimu lakini sasa ni maslahi ya wale waliofiwa na matakwa yao kuhusu mazishi yaendeshwe vipi.