1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Siku ya Watoto Ujerumani

Lillian Urio20 Septemba 2005

Leo hii Ujerumani inasherehekea siku ya watoto kitaifa. Wakati sherehe za kawaida zikiendelea wataalam wa watoto wanasema ni muhimu kwa wakati huu kuwafikiria watoto wanaoishi Ujerumani katika hali ambayo hairidhishi.

Watoto mjini Köln wakisherehekea siku ya Watoto
Watoto mjini Köln wakisherehekea siku ya WatotoPicha: dpa

Mashirikia yasio ya kiserikali yanayoshughulikia masuala ya watoto Ujerumani, pamoja na mashirika ya kimataifa, likiwemo shirika la Umoja wa Mataifa, UNICEF, yamesema nchini hapa kuna watoto wanaokuwa katika mazingira magumu na ni lazima jambo hili lizingatiwe.

Wanataka jamii ielewe suala hili na wamepanga kukutana katika lango la kihistoria la Brandenburger, mjini Berlin, watakuwa na kundi la watoto watakaokuwa wanafanya makelele wakitumia vifaa mbalimbali vya muziki, zikiwemo ngoma, kwa lengo la kuwaamsha watu wazima kwamba kuna watoto Ujerumani wanaoteseka.

Katika miaka ya karibuni hapa Ujerumani imekuwa jambo la kawaida kutokusikia makelele ya watoto wanaocheza barabarani, kama ilivyokawaida katika nchi nyingine, hasa zinazoendelea.

Hii ni kwa sababu idadi ya watoto wanaozaliwa nchini hapa inazidi kushuka sababu wanawake wengi zaidi, pamoja na wanaume, wanachagua kujiendeleza katika taaluma zao zaidi kuliko kuwa na familia.

Takwimu za Ujerumani zinaonyesha kwamba tofauti imekuwa kubwa kiasi kwamba kwa kila mtoto mmoja kuna takriban watu wazima wanne. Ukilinganisha na idadi ya magari, mjini Essen kuna magari matatu kwa kila mototo mmoja, mjini Hamburg ni magari manne na katika mji mkubwa wa kusini mwa Ujerumani wa Munchen ni magari matano.

Msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la masuala ya watoto, UNICEF, Bwana Rudi Tarneden, anasema kwa ujumla hali ya watoto wa Ujerumani ni nzuri ukilinganisha na ile ya watoto kwenye nchi maskini, lakini hairidhishi.

“Hali ilivyoUjerumani ni kwamba watoto hawahitaji kuhangaika sana ili waweza kuishi. Watoto wengi wanapata lishe bora na wanaenda shule. Pia mara nyingi unakuta wanavitu vya ziada kama vile michezo, nguo n.k. Lakini sasa hivi tunaona kuna mwelekeo mpya hapa Ujerumani wa ongezeko la umaskini baina ya watoto. Lakini hatumaanishi umaskini wa hali ya juu kama ilivyo katika baadhi ya nchi zinazoendelea.”

Hata jumuiya ya kulinda watoto ya Ujerumani inakubaliana na hili. Imesema karibu watoto milioni mbili wanaishi kutokana na misaada ya serikali, wengi wao na familia zao, na idadi hii inazidi kuongezeka. Ingawa watoto hawa hawashindi na njaa lakini kuna mambo fulani wanayokosa na hivyo wanakuwa tofauti na watoto wenzao.

Kwa mfano wanashindwa kushiriki katika mipango mbalimbali ya nje ya shule kama vile safari na michezo, kwa sababu wazazi au walezi wao hawawezi kuwalipia. Na baada ya shule watoto wenzao, hasa rika la vijana, wanapokutana katika migahawa wao inabidi wabaki nyumbani.

Matokeo yake pengo linatokea katika jamii kati ya watoto wanaokuwa katika familia zenye fedha na wale wanao kuwa katika familia za hali ya chini.

Pia kila mwaka watoto takriban 80,000 wanaondoka katika shule za sekondari bila ya kumaliza, wengi wao kutoka familia zinazopata misaada kutoka serikalini.