Silaha za nyuklia katika mataifa ya NATO
15 Oktoba 2010Ujerumani na Ufaransa zimetofautiana kuhusiana na kuwepo kwa silaha za nyuklia katika mataifa wanachama wa Jumuiya ya kujihami ya NATO. Mawaziri wa Ulinzi pamoja wa Mawaziri wa mambo ya nje wa mataifa 28 ya Jumuiya hiyo, wanakutana mjini Brussels kuzungumzia azimio la mkakati mpya wa ulinzi. Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Guido Westerwelle na mwenzake wa Ulinzi Karl-Theodor Zu Guttenberg walisema suala la kuachana na silaha za nyuklia linafaa kuwepo katika mkakati huo mpya. Pia walisema nchi kadhaa zinaunga mkono msimamo huo wao. Lakini Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa Herve Morin alipinga msimamo huo. Alishikilia kuwa Jumuiya hiyo ya NATO bado inahitaji kuwa na mfumo wa kujihami kutokana na silaha za nyuklia, msimamo ulioungwa mkono na Waziri wa Ulinzi wa Marekani Robert Gates. Mkakati huo mpya wa NATO utapitishwa katika mkutano wa utakaofanyika wiki ijaayo, mjini Lisbon Ureno.