Simba SC yalenga kuimarisha matokeo
17 Novemba 2025
Simba SC, ambao wamekuwa na rekodi nzuri kwenye Ligi ya Mabingwa, wameweka kambi maalum huku wakijikita zaidi kwenye kuongeza uimara ili kufanya zaidi kuliko misimu iliyopita.
Afisa habari wa Simba Ahmed Ally anatamba kuwa na kikosi Bora ambacho Mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kitacheza dhidi ya Petró Atlético de Luanda mchezo utapigwa Novemba 23, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa 10:00 jioni.
" Lazima Simba tuvuke kwenda hatua ya Robo fainali kwa sababu ya juhudi jitihada na ubora tulionao unataka utatoa alama tatu hutaki utatoa alama tatu Benjamin mkapa tutakupigia mpira mkubwa utatoa utaacha alama tatu Benjamin Mkapa”Amesema Afisa habari wa Simba Ahmed Ally
Kwa upande wa Yanga SC, wao wameendelea na mazoezi kuiwinda As Far Rabat katika mechi za makundi ya ligi ya mabingwa mchezo utakaochezwa Uwanja wa New Amaan Complex,Novemba 22 Zanzibar .
Afisa habari wa Yanga Ally Kamwe kuhusu maandalizi
"Unapocheza mechi za Ligi ya mabingwa maandalizi yake yanakuwa ya tofauti kabisa kocha wetu Pedro Goncalves yupo hapa kuhakikisha wachezaji wanaelewa wanachohitaji”Amesema Afisa habari wa Yanga Ally Kamwe.
Azam yaendelea kujiandaa
Azam FC nao hawako nyuma wapo wanajifua vyema kuelekea mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Maniema Union, utakaochezwa Novemba 23 nchini DR Congo kama anavyoeleza Afisa Habari wa Azam FC, Hasheem Ibwe
"wachezaji wetu baadhi ambao walikuwa majeruhi wameshapona wamebaki wawili Adolf pamoja na Cheickna Diakité wao wanaendelea na mazoezi ya pembeni lakini maandalizi ya klabu yapo vizuri As Maniema Union, ni Timu nzuri hatudhani kama mechi itakuwa rahisi Amesema Afisa Habari wa Azam FC, Hasheem Ibwe
Timu ya Singida Black Stars, wawakilishi wengine wa Tanzania kwenye Kombe la Shirikisho, wanatarajiwa kuondoka nchini kesho Novemba 18 kuelekea Algeria kwa ajili ya mchezo wao dhidi ya CR Belouizdad, utakaochezwa Novemba 22.
Beki wa Timu hiyo, Kennedy Juma ansema azma yao ni kuandika historia mpya.
"Mechi itakuwa ni ngumu wenyewe ni wakongwe katika mashindano haya lakini sisi ni mara yetu ya kwanza kucheza hatua ya makundi tutaenda kupambana kadri ya uwezo wetu ”Amesema Beki Kennedy Juma
Wadau wa soka nchini sasa wanatazama kwa hamu jinsi ambavyo maandalizi haya yatakavyozaa matunda, huku matumaini yakiwa juu kwamba msimu huu Tanzania itafanya historia katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho.
"Sisi tuna uwezo mkubwa sana wa kwenda robo fainali na sisi kuhusu kwenda robo fainali kwetu sio tatizo Kwanza tuna matumaini makubwa sana na Timu yetu tunaamini mwaka huu ni mwaka wetu na tunaweza kufanya vizuri sana kwenye hatua ya makundi”Wamesema Wadau wa soka