SINGAPORE: Ujerumani yapinga kiti kimoja kwa eneo la Euro
16 Septemba 2006Matangazo
Waziri wa fedha wa Ujerumani,Peer Steinbrück amepinga mashauri yaliyopendekezwa kuwa mataifa 12 yanayotumia sarafu ya Euro yawe na kiti kimoja katika bodi ya Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF.Mapendekezo hayo yametolewa kama sehemu ya mageuzi mbali mbali yanayofanywa katika taasisi hiyo.Waziri Steinbrück anaehudhuria mikutano ya mwaka ya IMF na Benki Kuu ya Dunia nchini Singapore amesema,Ujerumani ikishika nafasi ya tatu kiuchumi duniani,baada ya Marekani na Japan,lazima iendelee kuwa na usemi katika IMF. Hivi sasa shirika hilo linatafuta njia ya kuzipa nchi zinazonyanyuka kiuchumi,kama vile China, usemi zaidi katika uongozi wa taasisi hiyo yenye wanachama 184 na ambayo hutoa mikopo.