1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiSingapore

Singapore yamnyonga mtuhumiwa wa dawa za kulevya

Auleria Gabriel
28 Julai 2023

Singapore imemyonga mwanamke mmoja kwa kosa la kukutwa na dawa za kulevya, hiki kikiwa ni kisa cha kwanza katika kipindi cha takriban miaka 20.

Singapur | Protest gegen Todesstrafe
Mwanaharakati akiwa amevaa fulana yenye ujumbe wa kupinga hukumu ya kifo huko Singapore.Picha: Roslan Rahman/AFP/Getty Images

Saridewi Djamani mwenye umri wa miaka 45 amenyongwa nchini Singapore baada ya kukutwa na hatia ya kumiliki zaidi ya gramu 30 za heroin, kiwango ambacho ni zaidi ya mara mbili ya ujazo uliotajwa katika hukumu ya kifo nchini Singapore. Hukumu hiyo imetolewa siku ya Ijumaa, ikiwa ni ya kwanza kutolewa kwa karibu miongo miwili.

Licha ya upinzani kutoka kwa makundi ya kutetea haki za binaadamu, Singapore ni miongoni mwa nchi nne ambazo hivi karibuni zimewanyonga washtakiwa wengine kwa tuhuma kama hizo za kukutwa na dawa za kulevya. Watetezi hao wanadai kuwa hukumu ya kifo haiwezi kuzuia uhalifu.

Ofisi kuu ya Madawa ya Kulevya ya Singapore ilisema "Djamani amepewa adhabu hiyo kwa kuzingatia sheria," na kuongeza kuwa msamaha wake kutoka kwa rais pia ulikataliwa. Djamani alihukumiwa adhabu ya kifo mnamo Julai 2018. Rufaa yake dhidi ya kunyongwa ilitupiliwa mbali na Mahakama ya Rufaa mnamo Oktoba 2022. 

Singapore ni moja ya nchi yenye sheria kali zaidi dhidi ya dawa za kulevya ulimwenguni.Picha: ROSLAN RAHMAN/AFP

Singapore ni moja ya nchi yenye sheria kali zaidi dhidi ya dawa za kulevya ulimwenguni.

Shirika la habari la AFP likilinukuu Jeshi la Magereza la Singapore limesema, mnamo 2004, Yen May Woen alinyongwa kwa ulanguzi wa dawa za kulevya na tangu wakati huo, Djamani ndiye mwanamke wa kwanza kunyongwa. 

Soma pia: Mlanguzi mkuu wa madawa ya kulevya Colombia akamatwa

Djamani amekuwa mfungwa wa kumi na tano aliyehukumiwa kunyongwa tangu serikali iliporudisha adhabu ya kifo mnamo Machi 2022 baada ya kusimama kwa miaka miwili kutokana na janga la UVIKO-19.

Mfungwa mwingine wa dawa za kulevya anatarajiwa kunyongwa mnamo Agosti 3, 2023 hii ni kwa mujibu wa shirika la ndani la kutetea haki za binaadamu la Transformative Justice Collective.

Singapore ina mojawapo ya sheria kali zaidi za kupambana na dawa za kulevya duniani. Kusafirisha zaidi ya gramu 500 za bangi au zaidi ya gramu 15 za heroin kunaweza kusababisha hukumu ya kifo.

Licha ya kile ambacho mashirika ya haki za binadamu yanasema, Singapore inasisitiza kuwa hukumu ya kifo imesaidia kuifanya kuwa moja ya nchi salama zaidi barani Asia.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW