SIPRI: Bado Silaha za nyuklia zinatengezwa
18 Juni 2018Ripoti hiyo ya taasisi ya kimataifa ya utafiti wa masuala ya amani imesema idadi ya vichwa vya nyuklia imepungua kwa 470 ikilinganishwa na mwaka jana.
Punguzo hilo limetokana na mkataba uliofikiwa kati ya Marekani na Urusi mwaka 2010 ya kupunguza silaha za kinyuklia, mkataba unaojulikana START. SIPRI imeripoti kuwa nchi hizo mbili zenye nguvu zaidi duniani zinamiliki kwa pamoja asilimia 92 ya silaha za nyuklia zilizoko duniani.
Nchi zinatafuta silaha za kisasa
Ripoti hiyo imesema kuwa kufikia mapema mwaka huu, inakadiriwa kuwa Marekani ilikuwa na vichwa 6,450 vya nyuklia ilhali Urusi inamiliki 6,850. Nchi tisa duniani zinajulikana kuwa na silaha hizo za kinyuklia. Mbali na Urusi na Marekani nchi nyingine ni Uingereza, Ufaransa, China, India, Pakistan, Israel na Korea Kaskazini.
Mtafiti wa SIPRI Shannon Kile ameliambia shirika la habari la Ujerumani dpa kuwa licha ya kupungua kwa umiliki wa silaha za kinyuklia, bado kuna mambo ya kimsingi yanayoendelea kutia wasiwasi.
Kile amesema nchi zote zinazomiliki silaha hizo aidha zimeanza au kutangaza nia ya kuanza mipango ya muda mrefu ya kuzifanya silaha zao kuendana na teknolojia ya kisasa na hakuna hata moja inayojitayarisha kuanzisha mpango wa kuondokana kabisa na mpango wa kinyuklia katika siku za usoni.
Mojawapo ya mifano SIPRI imetoa ni Marekani ambapo wabunge wa nchi hiyo mwaka jana waliidhinisha mpango wa kuboresha silaha kutoka makombora na ndege za kivita hadi kutengeza vichwa vya nyuklia.
Inakadiriwa kuwa Marekani itatumia dola bilioni 400 kufadhili mpango huo kati ya mwaka 2017 hadi 2026.
Korea Kaskazini haiko wazi kuhusu silaha zake za nyuklia
Kile amesema Marekani iko wazi kuhusu mpango wake wa kinyuklia ila la kushangaza Ufaransa haiko wazi sawa na Urusi na China, licha ya kuwa Urusi inabadilishana na Marekani taarifa kuhusu silaha za kinyuklia chini ya mkataba wa START utakaodumu hadi mwaka 2021.
Nchi iliyotajwa na SIPRI kuwa isiyo na uwazi kabisa ni Korea Kaskazini inayokadiriwa kuwa na kati ya makombora 10 hadi 20 ya nyuklia. Uingereza inakadiriwa kuwa na 215, Ufaransa 300, China 280, India kati ya 130 hadi 140, Pakistan kati ya 140 na 150 na Israel ina makombora 80 ya baruti.
Kile amesema ni mapema mno kusema iwapo mkutano wa kihistoria kati ya Rais wa Marekani Donald Trump na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un utaifanya Korea Kaskazini kuwa wazi zaidi kuhusu mpango wake wa kinyuklia.
SIPRI imesema tukio lililowafurahisha lililofikiwa mnamo mwezi Septemba mwaka jana, ni kutiwa saini kwa makubaliano ya kupiga marufuku matumizi ya silaha za nyuklia, ambayo matokeo yake hayatakuwa ya haraka lakini itazishinikiza nchi zinazomiliki silaha hizo za kinyuklia kuachana nazo jinsi muda unavyokwenda.
Hadi sasa, ni nchi 59 zilizotia saini makubaliano hayo, lakini ni nchi kumi pekee zilizoyaidhinisha. Ili kuidhinishwa rasmi makubaliano hayo ya kupiga marufuku silaha za nyuklia, nchi 50 zinahitaji kuyaidhinisha rasmi.
Mwandishi: Caro Robi/dpa
Mhariri: Josephat Charo