1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

SIPRI: Biashara ya silaha iliongezeka 2015

5 Aprili 2016

Matumizi na manunuzi ya silaha yaliongezeka katika kipindi cha mwaka 2015 ikiwa ni mara ya kwanza katika kipindi cha miaka minne huku Marekani, China na Saudi Arabia zikiongoza katika orodha hiyo duniani kote

Waffenlieferung Somalia Beschlagnahmung Australien Navy
Picha: Reuters/S.Ebsworth/Australian Defence Force

Hiyo ikiwa ni kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na taasisi moja yenye makao yake nchini Sweden. Taasisi hiyo ya mjini Stockholm, Sweden inayohusika na utafiti katika masuala ya amani kimatifa-SIPRI, imekadiria kuwa kiasi cha dola trilioni 1.67 zilitumika katika manunuzi ya silaha katika kipindi cha mwaka 2015, ikiwa ni ongezeko la asilimia moja zaidi kulinganisha na kipindi cha mwaka 2014.

" Hii ni mara ya kwanza tangu mwaka 2011 kuwa na ongezeko la matumizi katika silaha" amesema Sam Perlo- Freeman ambaye ni mkuu wa kitengo kinachohusika na matumizi ya fedha kijeshi katika taasisi alipozungumza na shirika la habari la DPA.

Marekani bado imeendelea kuongoza katika matumizi ya fedha kwa ajili ya manunuzi ya silaha ikitumia kiasi cha dola bilioni 596 licha ya punguzo la asilimia 2.4 la matumizi hayo kila mwaka. Kiwango hicho kwa Marekani ni sawa na asilimia 36 ya matumizi ya manunuzi ya silaha duniani kote ambayo ni karibu ya mara tatu ya matumizi ya aina hiyo kwa China ambayo inashika nafasi ya pili.

Kiwango cha fedha kwa ajili ya manunuzi hayo kwa China kiliongezeka kwa asilimia 7.4 ukilinganisha na kile cha mwaka 2014, na kimekadiriwa kuwa dola bilioni 215 ikiwa ni mara ya nne ya zaidi ya kiwango cha fedha kinachotumiwa na mshindani wake India.

Mkurugenzi Mkuu wa SIPRI Dan SmithPicha: DW/T. Meheretu

Kwa mujibu wa taasisi hiyo ya SIPRI matumizi hayo ya China yalikuwa sawa na ya kipindi cha miaka iliyopita yakiendana sawa na kiwango cha kukuwa kwa uchumi wake. Mataifa ya Indonesia, Ufilipino na Vietnam nayo pia yameshuhudia ongezeko la matumizi ya fedha katika manunuzi ya silaha.

Saudi Arabia imeipiku Urusi katika matumizi hayo ikishika nafasi ya tatu, ambapo imetumia dola bilioni 87.2 katika kipindi hicho cha mwaka 2015. Matumizi ya fedha katika manunuzi ya silaha kwa nchi hizo mbili ambazo zina utajiri wa mafuta yamepungua kutokana na kushuka kwa bei ya mafuta katika soko la dunia.

Taasisi hiyo ya utafiti ya SIPRI inakadiria kuwa Urusi ilitumia karibu dola bilioni 66 katika matumizi ya kijeshi, ikiwa ni ongezeko la asilimia 7.5 ukilinganisha na mwaka 2014.

Mataifa mengine ambayo yanakamilisha idadi ya mataifa 10 yanayoongoza katika matumizi ya fedha kwa ajili ya manunuzi ya silaha ni pamoja na Uingereza, India, Ufaransa, Japan, Ujerumani na Korea Kusini.

Utafiti wa SIPRI umebainisha kuwa mgogoro wa Ukraine umechangia matumizi hayo kwa mataifa yanayopakana na Urusi ikiwemo Poland, Romania na mataifa ya Baltic. Mapambano dhidi ya kundi la Itikadi kali la Dola la Kiislamu nayo pia yametajwa kuchangia katika matumizi ya manunuzi hayo ya silaha.

Bara la Afrika limetajwa kushuka kwa kiwango cha matumizi ya fedha katika manunzi hayo huku taasisi hiyo ikishindwa kutoa mchanganuo wa matumizi hayo kwa matifa ya Mashariki ya Kati kutokana na kukosa data katika mataifa kadhaa ikiwa ni pamoja na Kuwait, Qatar, Syria, Umoja wa falme za kiarabu na Yemen.

Mwandishi: Isaac Gamba/ DPAE
Mhariri: Grace Patricia Kabogo