SIPRI: Matumizi ya fedha kijeshi yaongezeka
2 Mei 2018Taasisi hiyo ya kimataifa inayohusika na utafiti wa masuala ya amani inakadiria kiasi cha dola tirilioni 1.73 ziliwekezwa kwa ajili matumizi ya kijeshi pekee likiwa ni ongezeko la asilimia 1.1 kulinganisha na mwaka 2016 na hiyo ikimaanisha kuwa ni sawa na dola 230 kwa mtu mmoja.
Marekani imeendelea kuongoza kwa matumizi hayo ulimwenguni kote kwa kiwango cha dola bilioni 610 kiwango kinachoonekana kutobadilika mwaka hadi mwaka huku nchi hiyo ikihusishwa na zaidi ya robo ya matumizi ya fedha kijeshi duniani kote.
Akihojiwa na DW mtafiti mwandamizi wa taasisi ya SIPRI Pieter Wezeman amesema China ambayo inashika nafasi ya pili inakadiriwa kutumia kiasi cha dola bilioni 228 na matumizi yake yameongezeka kwa kiwango cha aslimia 5.6 ambacho ni cha juu katika kipindi cha kuanzia mwaka 2008.
Kwa upande mwingine Saudi Arabia imeshika nafasi ya tatu katika orodha hiyo ambayo awali ilikuwa ni nafasi ya Urusi na kwa mujibu wautafiti huo matumizi yake kijeshi yamefikia dola bilioni 69.4 kwa mwaka 2017.
Licha ya kushuka bei ya mafuta migogoro ya kivita inayoendelea Mashariki ya Kati imechochea matumizi ya fedha kijeshi katika kanda hiyo.
Matumizi ya Urusi kijeshi yapungua
Ripoti hiyo ya SIPRI inaonesha mtumizi ya Urusi kijeshi kupungua kulinganisha na mwaka 2016 ikiwa ni mara ya kwanza tangu mwaka 1998. SIPRI imehusisha kushuka kwa matumizi hayo na kuporomoka kwa bei ya mafuta.
Hata hivyo kujiboresha kijeshi bado kunaendelea kusalia kuwa kipaumbele cha Urusi.
India imeipiku Ufaransa katika matumizi hayo na kushika nafasi ya tano ambapo kwa mujibu wa utafiti huo inaonekana kutumia karibu dola bilioni 64.
Utafiti huo unaonesha kuwa mataifa manne miongoni mwa mataifa 15 yanayoongoza kwa matumizi hayo yanatoka barani ulaya. Mataifa hayo ni Ufaransa, Uingereza, Ujerumani na Italia.
Mataifa mengine ambayo ni mongoni mwa kundi la nchi hizo 15 ni pamoja na Japan, Korea Kusini na Australia.
SIPRI inasema Algeria inaendelea kusalia kuwa nchi yenye matumizi makubwa kijeshi barani Afrika lakini matumizi yake yalishuka katika mwaka 2017 kutokana na kushuka kwa bei ya mafuta na gesi.
Matumizi hayo yemeongezeka kwa zaidi ya asilimia 4 kwa nchi za Amerika ya Kusini huku Argentina na Brazil zikichochea matumizi hayo.
Kwa mujibu wa taasisi hiyo ya SIPRI matumizi hayo yamezingatia mishahara, gharama za uendeshaji , manunuzi ya silaha na vifaa vinginevyo pamoja na gharama za utafiti na maendeleo.
Mwandishi: Karsten Knipp-DW/DPAE
Mtafsiri: Isaac Gamba
Mhariri: Josephat Charo