SIPRI: Vita Ukraine vyapandisha faida ya wauza silaha
1 Desemba 2025
Pamoja na hayo ripoti ya Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Masuala ya Amani (SIPRI) yenye makao yake nchini Sweden imesema matatizo ya uzalishaji yaliathiri usambazaji wa silaha hizo.
Kwa mujibu wa SIPRI kiasi hicho kinaonekana kuwa cha juu kwa asilimia 5.9 kuliko mwaka uliopita, na katika kipindi cha 2015 hadi 2024, mapato ya watengenezaji 100 wakuu wa silaha yameongezeka kwa asilimia 26.
Katika taarifa hiyo, Lorenzo Scarazzato, mtafiti wa Programu ya Matumizi ya Kijeshi na Uzalishaji wa Silaha ya SIPRI, anaeleza "Mwaka jana mapato ya silaha duniani yalifikia kiwango cha juu zaidi kuwahi kurekodiwa na SIPRI, huku wazalishaji wakitumia fursa ya mahitaji makubwa.”
Ulaya kama kichocheo cha mauzo ya silaha
Jade Guiberteau Ricard, mtafiti wa programu hiyo hiyo, aliliambia Shiria la Habari la Ufaransa AFP kwamba imechochewa zaidi na Ulaya, ingawa ‘maeneo yote yameongezeka isipokuwa Asia na Oceania na kusema ongezeko la mahitaji barani Ulaya linahusiana na vita vya Ukraine na mtazamo wa tishio la Urusi kwa nchi za Ulaya.
Kwa mujibu wa SIPRI, mahitaji kutoka Ukraine pamoja na nchi zinazoiunga mkono kijeshi na ambazo zinahitaji kupanua upya akiba zao ya silaha yamechangia kuongezeka kwa mahitaji. Ricard aliongeza kuwa nchi nyingi za Ulaya sasa pia zinatafuta kupanua na kuboresha majeshi yao, ‘jambo ambalo limesababisha chanzo kipya cha mahitaji.
Marekani imepata mapato ya dola bilioni 334
Marekani ni makazi ya watengenezaji 39 kati ya 100 wakuu wa silaha duniani, wakiwemo watatu wa juu zaidi, Lockheed Martin, RTX (zamani Raytheon Technologies) na Northrop Grumman. Watengenezaji wa silaha wa Marekani walishuhudia mapato yao ya jumla yakipanda kwa asilimia 3.8 na kufikia dola bilioni 334 mwaka 2024, karibu nusu ya jumla ya dunia yote.
Wakati huohuo, waandishi wa ripoti walibainisha kuwa matumizi ya bajeti kupita kiasi na ucheleweshaji vinatatiza programu kadhaa muhimu zinazoongozwa na Marekani, kama ile ya ndege ya kivita ya F-35 na manowari za Columbia-class.
Matokeo ya vita vya Ukraine
Watengenezaji 26 kati ya 100 wakuu wa silaha walioko Ulaya ambao walishuhudia mapato yao ya jumla yakikua kwa asilimia 13 na kufikia dola bilioni 151. Kampuni ya Czech, Czechoslovak Group, ilishuhudia mapato yake yakipanda kwa asilimia 193 ongezeko kubwa zaidi kati ya wazalishaji100 wakuu na kufikia dola bilioni 3.6. Kampuni hiyo ilinufaika na mipango wake wa kusambaza silaha kwa Ukraine.
Watengenezaji wawili wa silaha wa Urusi pia wako miongoni mwa 100 wakuu, Rostec na United Shipbuilding Corporation, mapato yao ya jumla yalipanda kwa asilimia 23 hadi kufikia dola bilioni 31.2, licha ya upungufu wa vipengele kutokana na vikwazo vya kimataifa, kwa kuwa mahitaji ya ndani yalifidia kushuka kwa mauzo ya nje.
Wakati huohuo, kampuni tisa kati ya zile 100 kuu, ziko Mashariki ya Kati, zikiwa na mapato ya jumla ya dola bilioni 31. Kampuni tatu za Israel zilizoorodheshwa zilichangia zaidi ya nusu ya kiasi hicho, huku mapato yao ya jumla yakikua kwa asilimia 16 na kufikia dola bilioni 16.2.
Chanzo: AFP