Sisi atishia kuivamia Libya kijeshi
21 Juni 2020Kauli ya Sisi inakuja kukiwa na wasiwasi juu ya uingiliaji kati wa Uturuki nchini Libya, ambao umefanikiwa kumrejesha nyuma mbabe wa kivita, Jenerali Khalifa Haftar.
Sisi alitumia ziara yake kukagua vikosi vya jeshi la anga kwenye mpaka wa nchi yake na Libya, kuvionya vikosi vya serikali inayotambuliwa kimataifa nchini Libya, visijaribu kuvuuka mstari wa mbele wa mapigano kuelekea waliko waasi wanaoongozwa na Jenerali Haftar.
"Uingiliaji wa moja kwa moja kutoka dola la Misri sasa umepata uhalali wa kimataifa", Sisi aliwaambia waliohudhuria baada ya kukaguwa vikosi hivyo vya kijeshi, akiongeza kwamba Misri ina haki ya kujilinda baada ya vitisho vya moja kwa moja kutoka wanamgambo wa kigaidi na mamluki wanaoungwa mkono na mataifa ya kigeni, akimaanisha baadhi ya makundi yenye silaha yanayoiunga mkono serikali ya Libya na kusaidiwa na Uturuki.
Lengo kubwa la uingiliaji wowote itakuwa ni kuulinda mpaka wa kilomita 1,200 upande wake wa magharibi, kusaidia kusitishwa kwa mapigano na kurejesha amani na utulivu nchini Libya, alisema mwanajeshi huyo wa ngazi za juu, aliyegeuka kuwa rais baada ya kumpinduwa rais wa kwanza halali aliyechaguliwa kidemokrasia, Mohammed Mursi.
Uturuki yafanikisha mapambano
Msaada wa Uturuki kwa serikali ya Libya ulifanikiwa kuwarejesha nyuma waasi hao, ambao kwa miezi 14 walikuwa kwenye operesheni ya kuutwa mji mkuu wa Libya, Tripoli, wakiungwa mkono na Urusi, Muungano wa Falme za Kiarabu na Misri.
Kabla ya hotuba yake, Sisi alizungumza na marubani kadhaa wa jeshi la anga na vikosi maalum kwenye kituo hicho cha kijeshi, akiwaambia: "Kuweni tayari kutekeleza misheni, hapa ndani ya mipaka yetu, au ikilazimika hata nje ya mipaka yetu."
Muungano wa Falme za Kiarabu na Saudi Arabia zilielezea uungaji mkono wao kwa dhamira ya Misri kuilinda mipaka na usalama wake. Hakukuwa na kauli ya haraka kutoka Uturuki na Libya.
Misri yataka kusitishwa mapigano
Mapema mwezi huu, Misri ilitoa wito wa kusitishwa mapigano nchini Libya kama sehemu ya mpango wa amani na pia kuundwa kwa baraza la uongozi uliochaguliwa.
Ambapo Marekani, Urusi na Muungano wa Falme za Kiarabu waliuunga mkono mpango huo, Uturuki iliukosowa kuwa ni jaribio la kumnusuru Haftar kufuatia kushindwa kwake kwenye uwanja wa vita.
Siku ya Jumamosi (Juni 20), Sisi alisema nchi yake imekuwa ikisita kuingilia kijeshi nchini Libya na inataka suluhisho la kisiasa kwa mgogoro uliopo, lakini akiongeza kwamba "hali sasa ni tafauti."
"Ikiwa watu wengine wanadhani wanaweza kuvuuka mstari wa mbele wa Sirte-Jufra, huu ni mstari mwekundu kwetu," alisema mbele ya hadhira iliyojumuisha baadhi ya viongozi wa makabila ya Libya.
Sisi alizitaka pande hasimu kuheshimu mstari huo na kurejea kwenye mazungumzo, huku pia akiahidi kwamba Misri inaweza kuyapa makabila ya Libya mafunzo na silaha kupambana na "wanamgambo wa kigaidi."