1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

“Sisi pia ni Wamarekani“: Maisha na taswira ya Muislamu nchini Marekani baada Septemba 11

9 Agosti 2011

Tangu 9/11, Waislamu nchini Marekani wana matatizo kuhusu taswira yao. Baadhi yao wamejijumuisha vizuri kama watu binafsi. Wao hukabili waziwazi habari zisizovutia na hujitolea kusaidia katika jamii wanakoishi.

Nur für Projekt 9/11: Spurensuche USA

Kwa mujibu wa kituo cha utafiti wa masuala yanayohusika na dini na jamii, Pew Forum, hivi sasa kuna zaidi ya Waislamu milioni mbili na nusu nchini Marekani. Kawaida Waislamu hawa ni watu waliojijumuisha vizuri katika jamii, ni wasomi na mara nyingi ni watu wa tabaka la kati. Lakini tangu tarehe 11 Septemba 2001, wengi wao wanalalamika kuwa sasa maisha yamekuwa magumu. Habari zinazogonga vichwa vya habari huchochea midahalo ya umma, kama mabishano yaliyozuka kuhusu Kituo cha Kiislamu kinachotazamiwa kujengwa karibu na uwanja wa Ground Zero mjini New York.

Kwa hivyo, Waislamu wanajitahidi sana kuwaeleza wakaazi wenzao katika jamii kuwa wao, sawa na majirani zao wa Kikristo, wanapinga ugaidi unaofanywa na wafuasi wa itikadi kali za Kiislamu. Kwa mfano, katika kituo cha uongozi mjini Rockville katika jimbo la Maryland nchini Marekani, raia wamekusanyika katika chumba kikubwa kuzungumza pamoja na mbunge wao juu ya mchango unaotolewa na jamii ya Wamarekani wenye asili ya Kiasia. Samira Hussein aliyehudhuria kikao hicho anasema kuwa yeye anaunga mkono jamii zingine kama anavyoungwa mkono na jamii hizo. Lakini ilikuwa kazi ngumu hadi kufikia hapo.

Kuwa Muislamu nchini Marekani baada ya Septemba 11

Japo kuna ubapuzi, Samira Hussein hujishughulisha katika manispaa yakePicha: DW

Samira Hussein ni Mpalestina anaeishi katika wilaya ya Montgomery na ni Muislamu. Yeye alikwenda Marekani mwaka 1972 alipokuwa msichana. Ameolewa Marekani na amezaa watoto wanne. Anasema matatizo yalianza wakati wa vita vya kwanza vya Ghuba. "Mwanzoni waliharibu magari yetu. Walichana tairi za magari, walituvunjia milango, tulitupiwa taka na mizoga ya ndege na walichimbua mimea yetu. Baya zaidi ni kwamba kila siku watoto wangu walipigwa shuleni na walifuatwa njiani. Walitutukana na walitufanyia mambo mengi." Anasema Samira.

Mambo yalizidi kuwa mabaya kufuatia mashambulizi ya tarehe 11 Septemba 2001. Ghafla moja, Samira, ambaye anafanya kazi ya huduma za jamii, alijikuta yeye mwenyewe akibaguliwa hata kazini kwake. "Sikufanya kosa lolote. Ni raia ninayefuta sheria, najitolea shuleni na katika jamii. Bila ya kujali, kila wakati najaribu kutoa mchango wangu katika jamii. Lakini niliadhibiwa kwa vile mimi ni Mpalestina na Muislamu. Hiyo haikuwa haki." Anasema kwa masikitiko.

Samira aliamua kufanya kama hapo awali. Alijitolea zaidi: katika mikutano ya wazazi, skuli na katika jamii. Na mote aliwaeleza watu anaoukutana nao, imani yake na uzalendo wake. Kwenye skuli, aliwafafanulia wanafunzi aliokutana nao sababu za yeye kuvaa hijabu. "Silaha yangu ni elimu. Nataka kuwafahamisha binadamu na mahala bora pa kuanzia ni kwa watoto. Kwani mtoto anapoelewa utamaduni wetu na dini yetu, basi hata wazazi hubadili maoni yao." Anasema kazi hiyo imezaa matunda, kwani mwaka 2002 alitunukiwa zawadi na wilaya yake kwa jitahada za kupiga vita ubaguzi.

Muislamu anapopigania hadhi na nafasi yake Marakeni

Tufail Ahmad alizaliwa India, aliishi Pakistan na alihamia Marekani mwaka 1973. Sasa kampuni yake ya meli za kusafirishia mizigo, inaongozwa na mtoto wake mmoja wa kiume. Kama mzee katika jamii yake, aliguswa sana na mashambulizi ya Septemba 11, hasa kwa kuwa yalihusishwa na dini yake ya Uislamu. Akaamua kuwa angelifanya kila linalowezekana kurekebisha mahusiano yaliyoharibiwa na athari za mashambulizi hayo. Mwanzoni alifanya mipango ya kukutana na kujadiliana na watu wa imani yake na imani tofauti na baadaye akafanya mipango ya kukusanya misaada ya kunufaisha watu wote katika jamii.

Badminton huchezwa Juma-tano, Ijumaa ni SalaPicha: DW

Tangu mwaka 2001, Waislamu katika wilaya ya Montgomery hukusanya chakula kila mwaka kwa ajili ya kuwalisha wasioweza kujikimu. Ahmad haoni haya kusimama nje ya maduka makubwa na kuomba michango. Kwa njia hiyo, kila mwaka huweza kukusanya maelfu ya kilo za vyakula. Wamewahi hata kuchinja ng’ombe na kugawa nyama kwa watu wenye shida. "Katika jamii hii, wale waliokuwa wachache sasa ndio walio wengi. Lakini umeona kuwa kazi zote za kujitolea katika jamii zinafanywa na Wazungu?" Ahmad anajaribu kuibadili hali hiyo, akiamini kuwa ni kwa kufanya hivyo tu, ndipo Waislamu na makundi mengine ya wachache watakapoweza kujijumuisha nchini Marekani.

Mara nyengine Wamarekani hawaangalii dini ya mtu

Waled Hafiz ni Msyria. Aliishi Ujerumani kwa miaka 20, kabla ya kuhamia na kufanya kazi Marekani miaka 10 iliyopita. Yeye ni mwanachama katika Wakfu wa Waislamu katika wilaya ya Montgomery, ambalo ni shirika la Waislamu wanaofanya kazi za kujitolea katika jamii. "Katika eneo hili, watu wanajua zaidi kuhusu ulimwengu. Ukienda Texas au Virginia ya Magharibi, huko hawajui Syria iko wapi au Jordan na nani aliyehusika na mashambulizi ya Septemba 11. Wala hawataki kujua."

Kwa upande mwingine, kuna Mimi Hassanein ambaye anaona kuwa watu katika wilaya ya Montgomery wanamuunga mkono. Mmisri huyo mwenye miaka 63, ana skuli tatu za chekechea na moja ipo Germantown. Baada ya mashambulizi ya Septemba 11, alihofia kuwa wazazi wasingeliwapeleka watoto wao katika skuli zake. Lakini ilikuwa tofauti kabisa, kwani aliungwa mkono na wazazi hao. Mimi anasema kuwa watu hao hawakumtazama kama Muislamu bali kama Mimi Hassanein.

Mimi aliondoka Misri kwenda Marekani miaka 40 iliyopita. Tangu mwanzoni alijitahidi kujijumuisha katika jamii ya Kimarekani, lakini huku akidumisha mila na utamaduni wake, akitumia njia za kikwao kuutafsiri utamaduni wa Kimarekani. Kwa mfano, wakati wa sherehe za Halloween, huwa hatengenezi mavazi ya Halloween kwenye skuli zake, badala yake huwapikia watoto vyakula vitamu vya Kiarabu kama vile Bakalava. "Vyakula vina lugha moja ya kimataifa. Daima mtu anapaswa kutazama kile kinachotuleta pamoja na sio kinachotutenganisha." Anasema Mimi Hassanein.

"Mimi pia ni Mmarekani"

Guled Kassim anakubaliana na Mimi Hassanein. Guled anatoka Somalia na alikwenda Montgomery mwaka 1985 akiwa na umri wa miaka 10. Sasa ni rais wa taasisi ya Waislamu iliyo na wanachama 300 hadi 400 wanaofanya kazi za kujitolea katika jamii. Alipoulizwa iwapo kwanza anahisi kuwa ni Muislamu au Mmarekani, Guled aliyewahi kuwa mwanajeshi kwenye jeshi la Marekani, alijibu kuwa kama angelikuwa Mkristo, asingeulizwa suali hilo. Jawabu lake ni kwamba yeye ni wote wawili. Anasema watu wa kizazi chake hawana matatizo kusema "Mimi ni Mmarekani na Muislamu au ni Muislamu na Mmarekani. Si muhimu lipi linalotangulizwa".

Mwandishi: Christina Bergmann/ZPR

Tafsiri: Prema Martin

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW