Slomka apewa jukumu la kuiokoa Hamburg
18 Februari 2014Kocha Mirko Slomka ana vaa viatu vya Bert van Marwijk kocha ambaye amefutwa kazi na Hamburg SV siku ya Jumamosi baada ya kupata kipigo cha mabao 4-2 dhidi ya Eintracht Braunsweig timu iliyoko katika nafasi ya mwisho katika msimamo wa ligi ya Ujerumani Bundesliga.
Hamburg ikiwa na point 16 kibindoni inashika nafasi ya 17 ikiwa juu ya Braunsweig kwa point moja. Timu zote hizo ziliingia katika mpambano wa 21 wa Bundesliga siku ya Jumamosi zikiwania kujitoa kutoka katika eneo la hatari la kushuka daraja msimu huu.
Slomka ametangazwa rasmi kuwa kocha wa Hamburg leo Jumatatu na pia ataongoza mazowezi ya timu hiyo hii leo, ambapo katika mchezo wa 22 Jumamosi ijayo Mirko Slomka atajaribu kubadilisha majaliwa ya Hamburg kwa kibarua kigumu dhidi ya makamu bingwa wa Bundesliga Borussia Dortmund nyumbani.
Hamburg SV iliachana na kocha wake Bert van Marwijk baada ya kuwapo katika wadhifa huo kwa siku 143, baada ya vipigo mfululizo mara saba.
Timu hiyo ambayo ni moja kati ya timu zilizoanza katika ligi ya Bundesliga mwaka 1963 na haijashuka daraja tangu wakati huo lakini sasa imo katika hatari kubwa msimu huu kuchafua rekodi hiyo.
Ndipo uongozi wa timu hiyo ulipoamua kujaribu kubadilisha hali hiyo kwa kumwajiri kocha mpya, ambaye ana uzoefu katika bundesliga kama anavyosema mwenyekiti wa Hamburg SV , Varl Jarchow.
"Tumekaa na uongozi wote na kujadili hali na kwa mara nyingine tena tumefanya tathmini. Baada ya kipigo cha kufadhaisha sana dhidi ya timu iliyoko mkiani kabisa mwa msimamo wa ligi , tumekubaliana kwa kauli moja, kwamba tuachane na Bert van Marwijk pamoja na msaidizi wake."
Mafanikio kuelekea kucheza vikombe vya Ulaya
Pamoja na hayo katika mchezo wa 21 wa Bundesliga jana Jumapili Wolfsburg ilifanikiwa kupata ushindi muhimu wa mabao 2-1 dhidi ya Hertha BSC Berlin na kujizogeza hadi nafasi ya tano katika msimamo wa ligi , ikijiweka katika nafasi ya kucheza mwakani katika ligi ya Ulaya , Europa League na hata kujiweka katika nafasi nzuri ya kucheza katika Champions League pia. Robin Knoche wa Wolfsburg anathibitisha hilo.
"Points tatu ni muhimu kila wakati, hususan kuzipata ukicheza ugenini. Ndio, ni muhimu wakati zinapatikana dhidi ya timu ambayo ni jirani yako katika msimamo wa ligi. Tunafurahia , kwamba tumeweza kunyakua point zote tatu.
Licha ya kushindwa Hertha Berlin imo katika nafasi nzuri ya kundi la timu zinazoweza kucheza katika mashindano ya Ulaya ikiwa na points 31. Timu hiyo ilipanda msimu huu kutoka daraja la pili na inafanya vizuri katika Bundesliga hadi sasa.
VFB Stutgart nayo ikiwa ni kigogo cha soka nchini Ujerumani inajikuta pia katika hali ya kuporomoka katika msimamo wa ligi. Ikiwa ugenini dhidi ya Hoffenheim , Stuttgart imejikuta ikikubali kipigo cha mabao 4-1 , ikiwa ni kipigo cha sita mfululizo.
Bayern kama kawaida yake ilidhihirisha kuwa msimu huu haina mshindani baada ya kuikandika SC Freiburg kwa mabao 4-0 , wakati Borussia Dortmund yaonekana kuzinduka baada ya kupata ushindi tena wa mabao 4-0 dhidi ya Eintracht Frankfurt siku ya Jumamosi.
Nürberg ikaandika ushindi wake wa tatu tangu kuanza kwa awamu ya pili ya msimu huu wa Bundesliga kwa kuwaangusha majirani zao wa Augsburg kwa bao 1-0 katika mchezo wa vuta nikuvute jana Jumapili kama anavyosema mchezaji wa Nürnberg Josip Drmic.
Tumejaribu kuangalia jinsi timu ya Augsburg inavyofanyakazi uwanjani na leo tumeweza kuzima moto wao. Nafikiri kwa kupambana na kuonesha nia, kwamba tunataka kupata ushindi , mambo yametunyookea.
Katika ligi ya Uhispania , La Liga , jana Real Madrid ilipachika mabao 3-0 dhidi ya Getafe na kuiweka timu hiyo ya mjini Madrid katika nafasi sawa pamoja na Barcelona na Atletico Madrid juu ya msimamo wa ligi hiyo zikiwa zote na point sawa.
Mchezaji chipukizi Jese , ambaye alishika nafasi ya Cristiano Ronaldo , CR7 ambaye anatumikia adhabu ya kadi nyekundu , aliipatia Real bao la mapema baada ya dakika sita.
Hapo jana pia Athletic Bilbao ilikubali kipigo chake cha kwanza katika uwanja wake mpya Estadio San Mames cha mabao 2-1 dhidi ya Espanyol.
Na huko katika bara la Afrika michezo ya mtoano ya duru ya kwanza katika Champions League imekamilika mwishoni mwa juma hili na kama ilivyotarajiwa Young Africans ya Tanzania ilifanikiwa kusonga mbele kwa jumla ya mabao 12-2 dhidi ya Komorozine ya visiwa vya Comoro.
Pamoja na ushindi huo wa Dar Young Africans , lakini KMKM ya Zanzibar licha ya kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Dedebit ya Ethiopia imeyaaga mashindano hayo kwa kufungwa jumla ya mabao 3-2. KMKM ilifungwa katika mchezo wa kwanza nchini Ethiopia kwa mabao 3-0.
Gor Mahia ya Kenya inasonga mbele kwa ushindi jumla wa mabao 3-1 dhidi ya US Bitam ya Gabon licha ya kufungwa bao 1-0 jana.
ASFA Yennenga ya Burundi imepata nafasi ya kusonga mbele pia kwa ushindi jumla wa mabao 4-2 dhidi ya Diambars ya Senegal kwa mikwaju ya penalti baada ya timu hizo kufungana kwa bao 1-1 , ambapo Yennenga ilishinda mwishoni mwa juma nyumbani kwa bao 1-0 ambapö katika mchezo wa kwanza timu hiyo ilifungwa pia kwa bao 1-0 nchini Senegal .
Rayon Sports ya Rwanda ilitoka sare ya mabao 2-2 na AC Leopards ya Jamhuri ya Kongo na Leopards inasonga mbele kwa goli la ugenini baada ya sare hiyo.
Kampala City Council ni moja kati ya timu ya Afrika mashariki na kati kuweza kusonga mbele baada ya ushindi jumla wa mabao 3-2 dhidi ya El-Merrikh ya Sudan licha ya kufungwa mabao 2-1 mwishoni mwa juma.
Champions League bara la Ulaya
Michuano ya Champions League katika bara la Ulaya inaanza rasmi kesho Jumanne katika awamu ya timu 16 zilizosalia katika kinyang'anyiro hicho.
Kesho Jumanne(18.02.2014) Bayer Leverkusen ya Ujerumani inatiana kifuani ya Paris St. Germain ya Ufaransa , wakati huo huo Manchester City ikiikaribisha mjini Manchester FC Barcelona ya Uhispania .
Jumatano itakuwa zamu ya Arsenal ikijaribu kuipima ubavu FC Bayern Munich ya Ujerumani na AC Milan ikiwa na miadi na Atletico Madrid ya Uhispania.
Wiki ijayo ya tarehe 25 mwezi huu Zenit St. Petersburg ya Urusi itajaribu bahati yake dhidi ya makamu bingwa wa Champions League Borussia Dortmund , wakati Olympiakos Piräus inaisubiri Manchester United nyumbani. Galatasaray Istanbul ina miadi na kikosi cha Jose Mourinho cha Chelsea na FC Schalke 04 iko nyumbani ikiikaribisha Real Madrid pamoja na CR7 Cristiano Ronaldo.
Kocha wa Bayern Munich Pep Guardiola amekiri kuwa kuumia kwa wachezaji wote mawinga wa upande wa kushoto Xherdan Shaqiri na Frank Ribery ni pigo kwa mabingwa hao watetezi katika pambano lake la Champions League dhidi ya Arsenal London.
Mabingwa hao wa Ulaya wanakwenda mjini London kwa pambano la siku ya jumatano dhidi ya Arsenal katika awamu hii ya mtoano ya timu 16 zilizosalia katika kinyang'anyiro hicho.
Vita vya maneno
Wakati huo huo kocha wa Arsenal Arsene Wenger ameendeleza vita vya maneno na Jose Mourinho jana Jumapili, akiuita ukosoaji wa kocha huyo wa Chelsea kuwa ni matamshi ambayo ni ya kudhalilisha.
Siku ya Ijumaa , Mourinho amemueleza kocha huyo raia wa Ufaransa kuwa ni "mtaalamu wa kushindwa," kwa kwenda miaka tisa bila ya kupata taji lolote. Wenger alijibu shutuma hizo kwa kulipiza kisasi dhidi ya Liverpool kwa ushindi wa mabao 2-1 katika kombe la FA jana Jumapili.
Saa 24 baada ya shambulio hilo la maneno dhidi ya Wenger, kikosi cha Mourinho kilikubali kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya Manchester City katika robo fainali ya kombe la FA.
Michezo ya olimpiki ya majira ya baridi mjini Sochi.
Canada imeishinda Finland kwa mabao 2-1 katika mchezo wa magongo katika barafu jana Jumapili na kushika nafasi ya juu katika kundi B.
Wakati huo huo hali mbaya ya hewa imelazimisha kupangwa upya kwa michezo ya olimpiki ya Sochi leo na kuahirishwa kwa michezo mingine.
Mbio za wanaume ambazo zilicheleweshwa kuanzia jana zimeahirishwa tena leo hadi kesho Jumanne, na mchezo wa kuteleza wa snowboard umefutwa baada ya kucheleweshwa kwa siku kadha.
Hata hivyo waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Thomas de Maiziere ameonesha kufurahishwa kwake na ushindi wa wanariadha wa Ujerumani katika michezo hiyo ya Sochi.
"Kiwango ambacho kimeoneshwa hadi sasa cha kupata medali za dhahabu ni kizuri sana, kwa jumla ya medali zilizopatikana. Lakini michezo ya olimpiki bado haijamalizika."
Wakati huo huo safari ya Jamaica katika michezo hiyo inaonekana kugonga mwamba baada ya kikosi chake cha watu wawwili kinachoshindana katika mchezo wa kuteleza katika barafu katika kitoroli kushika nafasi ya mwisho katika michezo ya mwanzo.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre /dpae
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman