1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Slovakia haitaki tena Waislamu

8 Januari 2016

Waziri mkuu wa Slovakia Robert Fico amefafanua kwamba jamii mchanganyiko katika Ulaya sasa ni suala lililoshindwa. Serikali ya nchi hiyo haitawavumilia tena jamii ya Waislamu nchini Slovakia.

Slowakei Robert Fico Premierminister EU-Afrika Gipfel Malta
Waziri mkuu wa Slovakia Robert FicoPicha: imago/ZUMA Press

Tukio la kushambuliwa wanawake mjini Cologne wakati wa mkesha wa mwaka mpya limesababisha mataifa mengi jirani ya Ujerumani , ambayo yalikuwa yanapinga kwa nguvu zote kuingia kwa wakimbizi barani Ulaya , kupata sababu ya kuhalalisha msimamo wao huo. Mataifa hayo ni pamoja na Slovakia na Poland.

Slovakia imetangaza kwamba haitachukua tena mkimbizi ambaye ni Muislamu. Hali kadhalika na Poland.

Eneo la kituo kikuu cha treni mjini Köln ambako genge la wanaume liliwavamia wanawakePicha: Reuters/W. Rattay

Waziri mkuu wa Slovakia Robert Fico amethibitisha kwamba anajisikia yuko sahihi katika msimamo wake. Amesema mtazamo wake mkali kuhusiana na sera za wakimbizi na watu wanaoomba hifadhi ni sahihi kabisa. Baada ya matukio mjini Cologne hakuna tena njia nyingine, anafafanua waziri mkuu huyo wa Slovakia.

"Hatutaki kitokee nchini Slovakia kitu kama kilichotokea mjini Cologne. Kwamba mtu anayeendesha maisha yake tofauti kabisa na sisi anafikiri anaweza kuwadhalilisha wanawake wetu hadharani."

Utamduni wa jamii mchanganyiko umekufa

Ni makosa makubwa, kudhania kwamba wakimbizi ambao ni wa dini nyingine wanaweza kujumuika kirahisi. Utamaduni wa ukarimu wa kuwakaribisha watu katika bara la Ulaya umekufa, kimesema chama kinachotawala nchini Slovakia cha Social Democratic.

Eneo la kituo kikuu cha treni mjini KölnPicha: picture-alliance/dpa/M. Hitij

"Serikali ya Slovakia ina hakika kwamba , fikira za kuwa na Ulaya yenye mchanganyiko wa tamaduni haiwezekani. Ni suala la kufikirika tu. Haiwezekani katika hali halisi."

Kuna hali inayoshabihiana kati ya wimbi la wakimbizi na mashambulizi ya mjini Paris na matumizi ya nguvu yaliyoonekana mjini Cologne, amesema waziri mkuu Fico, na kuongeza kuwa Umoja wa Ulaya umeshindwa kutambua hatari iliyopo.

Kila mara Umoja wa Ulaya umekuwa ukitetea kiwango cha mgao wa wakimbizi kwa kila nchi.

Katika wiki zilizopita Slovakia iliwachukua Wasyria Wakristo 146 kutoka Iraq bila kujiuliza mara mbili. Nchi hiyo ndogo mwanachama wa Umoja wa Ulaya hata hivyo haijaguswa hadi sasa na mzozo huu wa wakimbizi. Katika mwaka uliopita watu 167 walijiandikisha kutaka hifadhi, lakini ni wanane tu waliokubaliwa.

Polisi wakilinda usalama siku ya mkesha wa mwaka mpya mjini KölnPicha: picture-alliance/dpa/O. Berg

Poland nayo lawamani

Kwa upande wake serikali mpya ya Poland nayo inatumbukia katika ukosoaji mkubwa katika bara la Ulaya. Pia Hungary inashutumiwa kutokana na kuuvunja msingi wa maadili ya bara la Ulaya.

Wanawake waliandamana kupinga tukio la kunyanyaswa kingono wanawakePicha: Reuters/W. Rattay

Jamhuri ya Cheki hali kadhalika inakabiliwa na lawama za kuutumbukiza Umoja wa Ulaya katika kina kirefu. Kwa kuonesha wazi chuki dhidi ya Uislamu rais Milos Zeman wa nchi hiyo anapalilia chuki dhidi ya wakimbizi. Ametoa tahadhari juu ya hatari inayoikabili jamii ya watu wa nchi hiyo ya kusilimishwa.

Hata hivyo jana kansela wa Ujerumani alitoa kauli kali kuhusiana na mashambulio dhidi ya wanawake wakati wa mkesha wa mwaka mpya mjini Cologne. akizungumza na waandishi habari jana mjini Berlin Merkel amesema uhalifu huo haukubaliki.

Mwandishi: Heinlein , Stefan / ARD Prag / Sekione Kitojo

Mhariri: Daniel Gakuba.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW