1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Snowden aendelea kusubiri uwanja wa ndege

Admin.WagnerD25 Julai 2013

Mfichuaji wa siri za kijasusi za Marekani Edward Snowden, anaendelea kusubiri kibali cha kuondoka katika uwanja wa ndege mjini Moscow, huku Marekani ikizidisha shinikizo kwa Urusi kumrudisha nyumbani.

Snowden mjini Moscow.
Snowden mjini Moscow.Picha: picture-alliance/dpa

Taarifa zilizotolewa siku ya Jumatano zilionyesha kuwa maafisa wa serikali ya Urusi walikuwa wanajiandaa kumruhusu Snowden aondoke kutoka eneo la kusafiria la uwanja wa ndege wa Sheremetyevo, lakini katika mazingira ya kutatanisha, hakutokea. Snowden ameomba hifadhi ya kisiasa nchini Urusi na kwa sasa anasubiri kupatiwa hati itakayomuwezesha kuvuka mpaka na kuingia nchini Urusi kwa uhuru wakati maombi yake yakishughulikiwa --- hatua ambayo serikali ya Marekani imesema itakuwa inasikitisha sana.

Wakili wa Snowden, Anatoli Kutscherena.Picha: picture alliance/AP Photo

Waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei Lavrov alizungumza jana na waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry kuhusiana na suala la Snowden, lakini haikubainika wazi kama mazungumzo yao yalikuwa na athari yoyote kwa hatma ya mtoro huyo. Utawala mjini Washington unataka kumshtaki wakala huyo wa zamani wa shirika la usalama wa taifa NSA kwa kufichua taarifa za programu za uchunguzi za Marekani, lakini Moscow imekataa wito wa marekani kumkabidhi.

Marekani inataka Snowden arejeshwe
Balozi wa Marekani nchini Urusi alirejelea wito wa serikali yake kwa utawala mjini Moscow kumkabidhi Snowden, licha ya kutokuwepo makubaliano ya kukabidhiana watoro baina na mataifa hayo mawili. Balozi Michael McFaul ameandika kwenye mtandao wake wa Twitter asubuhi ya leo, kuwa Marekani haiiombi Urusi kumkabidhi Snowden, bali kumrudisha tu, na kuongeza kuwa Marekani imerudisha watu wengi nchini Urusi.

Wizara ya mambo ya kigeni ya Urusi haikutamka chochote kuhusu Kerry na Lavrov kuzungumzia hatma ya Snowden, zaidi ya kusema kwenye mtandao wake kuwa wanadiplomasia hao wawili walizungumzia uhusiano kati ya mataifa yao na hali ya mambo nchini Syria. Lakini msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani Jen Psaki, aliwaambia waandishi wa habari kuwa Kerry alimpigia simu Lavrov, baada ya kusikia kuwa Snowden angepatiwa hati ya muda kumruhusu kuondoka katika eneo la kusafiria la uwanja wa ndege.

Uwanja wa ndege wa Scheremetyevo mjini Moscow, anakoendelea kukwama Snowden.Picha: Kirill Kudryavtsev/AFP/Getty Images

Sheria za kimataifa zamkinga Snowden
Msemaji huyo alisema hatua yoyote ya kumruhusu kuondoka katika uwanja wa ndege itakuwa inasikitisha sana, na kuongeza kuwa imani yao ni kwamba sehemu pekee anakopaswa kuelekea ni Marekani. Lakini afisa wa juu wa haki za binaadamu nchini Urusi, Mikhail Fedotov, ameliambia shirika la habari la Urusi Interfax, kuwa itakuwa vigumu sana kumkabidhi Edward Snowden kwa Marekani, kwa sababu mikataba ya kimataifa hairuhusu kumkabidhi mtu alieomba hifadhi ya muda.

Fedotov aliongeza kuwa kwa kuwa Snowden bado yuko katika eneo ya kusafiria la uwanja wa ndege wa Sheremetyevo, utawala mjini Moscow hauwezi kumkabidhi kwa sababu kisheria hayuko nchini Urusi. Inaaminika Snowden amekuwa akiishi katika uwanja wa ndege tangu tarehe 23 Juni, baada ya kuwasili akitokea mjini Hong Kong.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/afpe, dpae
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW