Snowden hajulikani aliko
25 Juni 2013Matamshi hayo makali kutoka wizara ya mambo ya nchi za nje ya China sawa na mengineyo kama hayo yaliyotolewa hapo awali na vyombo vya habari vya nchi hiyo yanatishia kuzidi kuvuruga uhusiano kati ya nchi hizo mbili tangu Edward Snowden,anaesakwa na serikali ya Marekani kwa madai ya upelelezi kuihama Hong Kong jumapili iliyopita.
Ikulu ya Marekani inasema uamuzi wa maafisa wa serikali ya China kumruhusu Snowden aondoke ulikuwa wa makusudi,uliolengwa kumwachia mtoro huyo licha ya waranti unaotaka akamatwe.Uamuzi huo utakuwa na madhara katika uhusiano katika uhusiano kati ya China na Marekani" Ikulu ya Marekani imesema.Matamshi kama hayo yametolewa pia na waziri wa mambo ya nchi za nje John Kerry
China inasema tuhuma hizo hazina msingi na hazikubaliki
China imepinga lawama hizo."Lawama za Marekani hazina msingi na hazikubaliki hata kidogo."Amesema msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje Hua Chunying aliyeutetea pia uamuzi wa serikali ya Hong Kong kumuachia aondoke akisema "uamuzi huo unaambatana moja kwa moja na sheria."
Lawama kama hizo zimetolewa pia na Marekani dhidi ya Urusi.Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi Sergei Lavrow amesema Urusi haihusiki hata kidogo na mpango wa kutoroka Edward Snowden.Serguei Lavrow ameongeza kusema tunanukuu:Amefuata njia yake mwenyewe.Tumepata habari kupitia vyombo vya habari.Na hajavuka mpaka wa Urusi." amesema waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi Serguei Lavrow wakati wa mkutano na waandishi habari pamoja na waziri mwenzake wa Algeria.Tunaziangalia lawama dhidi yetu kuwa hazina msingi na hazikubaliki-mwisho wa kumnukuu.
Kitandawili cha wapi anakutikana kijana huyo bado hakijafumbuliwa.
Katika wakati ambapo duru kadhaa zinasema ameelekea Moscow,hakuna aliyemuona sio katika kituo cha ukaguzi wa paspoti katika uwanja wa ndege wa Moscow-Cheremetievo na wala si katika hoteli ya eneo la mpito katika uwanja huo wa ndege.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters/AFP
Mhariri:Yusuf Saumu