1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Solskjaer amsifu de Gea akisema ni "kipa bora duniani."

30 Septemba 2021

Meneja wa Manchester United Ole Gunnar Solskjaer amemsifu David de Gea na kudai kuwa ni "kipa bora duniani. Manchester United ilipata ushindi wake wa kwanza katika michuano ya ligi ya mabingwa dhidi ya Villarreal.

UEFA Champions League | Manchester United v Villarreal
Picha: ANTHONY DEVLIN/AFP/Getty Images

Solskjaer amesema kuwa Muhispania huyo aliwaokoa katika ushindi wa 2-1 katika mechi ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Villarreal jana Jumatano iliyochezwa ugani Old Trafford japo alikiri kwamba Villarreal walionesha mchezo mzuri katika kipindi cha pili.

Meneja huyo wa Manchester United alisema ushindi wao ulichangiwa pakubwa na ustadi wa David de Gea.

"Katika mechi hii alipata matokeo aliyostahili, kwa sababu alituokoa usiku wa leo. Tunapaswa kuwa wakweli na kusema hivyo,"alisema Solskjaer.

Katika kipindi cha kwanza, Villarreal ilionekana kudhibiti mechi hiyo, huku wakipata nafasi kadha za kufunga lakini David de Gea alionekana imara langoni na kuwanyima wageni hao nafasi baada ya kupangua mikwaju ya Arnaut Danjuma, Paco Alcacer na Yeremi Pino.

Soma pia: Rashford alalamikia ubaguzi wa rangi

Hata hivyo, Villareal inayoongozwa na Unai Emery ilipata bao lao kunako dakika ya 53 kupitia mshambuliaji Paco Alcacer, dakika saba baadaye United ilisawazisha bao hilo kupita shuti kali la mchezaji Alex Telles naye Cristiano Ronaldo akafunga bao la pili na la ushindi kunako dakika za mwisho za mchezo na kusisimua mashabiki ndani ya uwanja wa Old Trafford.

Solskjaer alimmiminia sifa Ronaldo, ambaye ni mshindi mara tano wa taji la mchezaji bora duniani Ballon d'Or, na kumtaja kama mchezaji mwenye ukomavu.

"Ndio kawaida yake na ameonesha hivyo kila mara - ana ukomavu wa kiakili, hapotezi dira kwenye mchezo, nimemwona siku nzima leo, jinsi alivyojipanga kwenye mchezo huo, na baadaye kutizimiza lengo lake."

Manchester United, ambayo ilipoteza mchezo wake wa kwanza dhidi ya Young Boys ya Uswizi, iko katika nafasi ya tatu kwenye kundi F ikiwa na alama tatu baada ya mechi mbili.

Soma pia:Ronaldo asema viwanja vitupu ni kama sarakasi bila wachekeshaji

Timu hiyo itaingia tena uwanjani Jumamosi hii Oktoba 2 kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Premia dhidi ya Everton ugani Old Trafford.

United na Everton zimeshikilia nafasi ya nne na tano mtawalia kwenye jedwali la ligi ya Premia zikiwa na alama 13 kila mmoja, japo United iko juu kwa tofauti ya magoli.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW