Somalia lazima imalize kipindi cha mpito
26 Julai 2012Baraza hilo limeitaka serikali ya mpito pamoja na viongozi wa siasa nchini Somalia kuongeza juhudi na kutimiza matakwa yote yanayotakiwa kufikia tarehe 20 mwezi ujao (Agasti) ambao ndio muda wa mwisho uliopangwa.
Somalia imekuwa na serikali ya mpito tangu mwaka 2004 lakini haijapata serikali kamili tangu mwaka 1991. Baraza la usalama lilitangaza tarehe hiyo mwezi Februari na kutoa wito kwa pande zote kutimiza makubaliano hayo yenye lengo la kuimarisha hali ya usalama, kuunda serikali kuu, pamoja na kuandika katiba.
Baraza hilo limeukaribisha mkutano wa bunge uliofanyika jana. Bunge la Katiba la Somalia lilikutana mjini Mogadishu hapo jana baada ya kuwa limeahirishwa mara kadhaa huko nyuma.
Kikao cha kwanza cha Bunge
Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi, Abdullahi Osman, amesema kuwa wajumbe wote 825 walioteuliwa kupitisha katiba walihudhuria. Wengine waliohudhuria kikao cha jana ni Rais Sheikh Sharif Sheikh Ahmed, Waziri Mkuu Abdiweli Mohamed Ali na Spika Sheikh Sharif Hassan Aadan.
Wengine waliohudhuria kikao cha ufunguzi wa Bunge hilo ni Mwakilishi Maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa Somalia, Balozi Augustine Mahiga, na wawakilishi wa Shirika la Maendeleo la Pembe ya Afrika, Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na balozi zote mjini Mogadishu.
Balozi Mahiga amesifu hatua hii. "Inatia moyo kuona kwamba mafanikio yameanza kupatikana. Hii ni hatua muhimu kuelekea mwisho wa kipindi cha mpito ambayo itaipa Somalia serikali imara na ya kueleweka baada ya kipindi cha miaka 21 ya mtikisiko wa kisiasa." alisema Balozi Mahiga.
Kikao hicho kinaendelea kufanyika kwenye chuo cha polisi cha Somalia mjini Mogadishu na kinatarajiwa kuendelea kwa siku wiki nzima. Ufunguzi wa bunge hilo unakuja baada ya viongozi wa makabila waliopewa jukumu la kuchagua wajumbe kushindwa kufanya hivyo mara kadhaa.
Hali ya usalama imeimarishwa
Wakati huo huo, vikosi maalumu vya usalama vimewekwa kuzunguka mji wa Mogadishu ili kudumisha usalama wa mji huo wakati wote wa vikao vya bunge, kwa mujibu wa Shirika la Habari la Somalia.
Vikosi vya ulinzi vimewekwa katika barabara inayotoka uwanja wa ndege wa Mogadishu kuelekea kasri ya rais, umbali wa kilomita 4, makutano matano ya barabara na maeneo yanayozunguka mahala ambapo Bunge linakutana. Vizuizi vya barabarani vimewekwa kwa ajili ya magari yanayoingia na kuondoka mjini huo na vinaangalia pia yale yaliyowekwa kinyume na sheria karibu na eneo la mkutano.
Msemaji wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika, Kanali Ali Aden Hamud, amesema kwamba vikosi vya Umoja wa Afrika vinalinda usalama wa ukumbi wajumbe wanapofanya mkutano.
Katika taarifa yake iliyoitoa jana, Baraza la Usalama pia limetoa wito wa kusitishwa kwa matumizi mabaya ya fedha za umma kwa kuimarishwa uwazi kwenye masuala hayo.
Ripoti ya Umoja huo iliyovuja hivi karibuni ilisema kuwa asilimia 70 ya fedha za umma nchini Somalia zimeibiwa au kutumiwa vibaya. Rais Sharif amenyooshewa kidole na ripoti hiyo pamoja na waziri wake mkuu, na spika wa bunge.
Mwandishi: Stumai George/AFP/AP
Mhariri: Mohammed Khelef