Somalia: Maelfu wakosa pa kulala baada ya makaazi kuchomwa
30 Januari 2018Uchambuzi wa shirika hilo wa picha za satelaiti unaonyesha kuwa kati ya Desemba 29 na Januari 19, 2018, takribani mabanda 3,000 yalivunjwa au kuharibiwa kwa kutumia mashine nzito.
Somalia ina wakimbizi wa ndani wapatao milioni 2.1, ambao nusu yao walikimbia mgogoro na ukame katika mwaka wa 2017 pekee. Wengi wao wanaishi katika makaazi yasiyo rasmi katika maeneo ya mijini.
Huma Rights Watch inasema tangu mwaka 2011, imeorodhesha matukio kadhaa ya ukiukwaji mkubwa dhidi ya ja,ii za watu waliokosa makaazi mjini Mogadishu, ikiwemo uhamishaji wa laazima, unyanyasaji wa kingono kwa kutumia nguvu na ubaguzi kwa misingi ya ukabila.
Serikali pamoja na sekta binfasi zinaripotiwa kuzihamisha jamii kwa nguvu bila kuwapatia njia yoyote mbadala. Shirika la Norway linaloshughulikia wakimbizi NRC, limeorodhesha visa 153,000 vya uhamishaji watu kwa nguvu mwaka 2017.
HRW yaitaka serikali ifanye uchunguzi
Januari 17 mwaka huu waziri wa mipango, uwekezaji na maendeleo wa Somalia Gamal Hassan, alijibu ukosoaji unaozidi kutoka mashirika ya misaada na kutangaza kuwa serikali ingechunguza uondoaji huo wa watu kwa nguvu.
Mtafiti wa Afrika katika shirika la Human Rights Watch Laetitia Bader, aliitaka serikali kufanya uchunguzi juu ya ukiukaji huo wa haki.
"Ni muhimu kwa serikali kutimiza wajibu wa kuchunguza jukumu la vikosi vya usalama katika uondoaji huu, kufahamu hasa nani aliagiza uondoaji huu kufanyika, na kuja na mapendekezo thabiti juu ya namna ya kuepusha ufukuzaji kama huo unaokiuka sheria kufanyika tena katika siku za usoni," alisema Bader katika mazungumzo na DW kwa njia ya simu.
Waathirika wa uondoaji huo wa nguvu waliozungumza na HRW walisema vikosi vya usalama viliharibu mabanda yao bila onyo, wakitumia vitisho na wakati mwingine nguvu kuwashinikiza waondoke nyumbani kwao. Uhamishaji huo uliwaacha bila maji, chakula au msaada.
Maelezo ya mashirika ya misaada yaliwiana na maelezo yao, inasema Human Rights Watch.
Wakaazi wanasema asubuhi ya Desemba 29, Polisi wa Somalia, maafisa wa shirika la upelelezi NISA, na vikosi vya jeshi waliwasili na kuzizingira kambi hizo na, wakitumia mabuldoza, walianza kuvunja mabanda yao karibu na barabara kuu.
Mwanamke mwenye umri wa miaka 56 alisema alipoamka mapema asubuhi askari wa polisi, jeshi na upelelezi walikuwa tayari wamezingira kambi yao ya Nuurto 2 na kuanza kuvunja vibanda vyao.
Wajibu wa serikali juu ya waliokosa makaazi
Chini ya Mkataba wa Kampala wa Umoja wa Afrika kuhusu ulinzi na msaada kwa watu walioppteza makaazi, ambao Somalia imeuidhinisha lakini bado kuuwasilisha kwa Umoja wa Afrika, serikali ina wajibu w akuwalinda watu waliopoteza makaazi dhidi ya kurudishwa kwa nguvu au kuhamishiwa katika eneo lolote ambako maisha yao, usalama, uhuru au afya vinaweza kuwa hatarini.
Baadhi ya waliohamishwa kwa nguvu walikuwa kwenye eneo linalohusika katika kesi ya mahakamani kati ya wamili wawili wa ardhi.
Tathmini ya kibinadamu ilibaini kuwa wakati baadhi ya wakaazi walipewa onyo siku kadhaa kabla ya uvunjaji huo, wale waliohojiwa na Human Rights Watch walisema hawakupewa taarifa, na kwamba maafisa pamoja na vikosi vya usalama walioshiriki katika uvunjaji huo hawakuwapa muda wa kutosha kuweza kukusanya vitu vyao na kutafuta makazi mbadala.
Ripoti ya tathmini inaonyesha kuwa familia 5,800 zililaazimishwa kuondoka, na kuwaacha watu 34,000 wakikosa mahala pa kukaa, na makaazi 25 yakichomwa moto. Tathimini nyingine iligundua kwamba vifaa vya maelfu ya dola vya elimu, usafi na maji viliharibiwa katika operesheni hizo.
Kwa mujibu wa tathmini ya NRC, wengi wa waliondolewa kwa nguvu walikuwa hawapati huduma nzuri za maji safi na usafi, na chini ya nusu ya waliohojiwa na baraza hilo la wakimbizi la Norway hawakuwa na mahala pa kukaa kabisaa, na hususani famili zinazoongozw na wanawake.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/HRW
Mhariri. Saumu Yusufu