Somalia na Ethiopia kurejesha uhusiano wa kidiplomasia
12 Januari 2025Somalia na Ethiopia zimetangaza Jumamosi kuwa zitarejesha uhusiano kamili wa kidiplomasia kufuatia ziara ya rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud aliyoifanya mjini Addis Ababa, ili kumaliza mpasuko wa mwaka mzima uliotishia kukosekana kwa utulivu katika Pembe ya Afrika.
Katika taarifa ya pamoja, Rais Mohamud wa Somalia na Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, walikubaliana kuimarisha uhusiano wa pande mbili kupitia uhusiano kamili wa kidiplomasia katika miji yao mikuu.
Soma: Marekani yapongeza mkataba mpya kati ya Ethiopia na Somalia
Ethiopia isiyozungukwa na bahari, imekuwa na shauku ya ufikiaji bahari, hali iliyoongeza malalamiko ya muda mrefu kati ya majirani hao wawili.
Somalia ilikasirishwa na hatua ya Ethiopia ya kusaini mkataba, mwaka mmoja uliopita na jimbo lake lililojitenga la Somaliland, ikiripotiwa kutambua uhuru wake kwa kubadilishana bandari na kambi ya kijeshi katika Bahari ya Shamu.