1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroSomalia

Somalia na Ethiopia zafanya mazungumzo Uturuki

2 Julai 2024

Somalia na Ethiopia zilifanya mazungumzo Jumatatu nchini Uturuki katika juhudi za kutuliza mivutano inayozidi kuongezeka baina ya nchi hizo mbili hasimu katika Pembe ya Afrika.

Mkutano wa AU - Rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud akiwa mjini Addis Ababa
Rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud akihudhuria mkutano wa Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa, Ethiopia: 17.02.2024Picha: REUTERS

Majirani hao wawili wana historia ya mivutano katika mahusiano yao ambapo migogoro ya kugombea maeneo yalipelekea kupigana vita viwili mwishoni mwa karne ya 20. Lakini kiini cha mzozo wa hivi karibuni ni makubaliano kati ya serikali mjini Addis Ababa na eneo la  Somaliland.

Chini ya mkataba huo uliosainiwa mwanzoni mwa mwaka huu, Somaliland ilikubali kukodisha karibu kilomita 20 ya eneo la pwani yake kwa miaka 50 kwa Ethiopia, ambayo ililenga kutumia eneo hilo kuanzisha kituo cha jeshi la majini pamoja na bandari ya kibiashara.

Pwani ya Somaliland katika eneo la BerberaPicha: Eshete Bekele/DW

Kufuatia makubaliano hayo ya mwezi Januari, Somaliland ambayo ilijitangazia uhuru wake kutoka Somalia mwaka 1991, ilidai kuwa Ethiopia ingeliitambua rasmi kama nchi huru, ingawa madai hayo hayakuthibitishwa na serikali mjini Addis Ababa.

Soma pia: Mzozo waifanya Somalia kutishia kuwatimua wanajeshi wa Ethiopia

Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Hakan Fidan aliwaleta pamoja mawaziri wenzake kutoka Somalia Ahmed Moallim Fiqi na yule wa Ethiopia Taye Atske Selassie kwa mazungumzo mjini Ankara.

Waziri Fidan aliwaeleza waandishi wa habari kwamba viongozi wa nchi hizo mbili wamekubaliana kuendeleza mazungumzo kwa nia ya kutatua masuala yanayozozaniwa na kuhakikisha utulivu wa kikanda, na kuongeza kuwa wamepiga hatua kubwa na kwamba anayo matumaini kwa siku zijazo.

Somalia na Ethiopia zaishukuru Uturuki 

Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Hakan FidanPicha: Murat Gok/Anadolu/picture alliance

Katika taarifa ya pamoja, mawaziri hao wa mahusiano ya kigeni wa Somalia na Ethiopia walithibitisha nia yao ya kutatua tofauti zao kwa njia ya amani, huku wakiishukuru Uturuki kwa upatanishi pamoja na mchango wake wenye nia ya kujenga.  Somalia na Ethiopia zilikuwa na mahusiano ya amani kabla ya Addis Ababa kusaini mkataba huo wenye utata na taifa lililojitenga la Somaliland.

Duru ya pili ya mazungumzo inatarajiwa kufanyika tena mjini Ankara ifikapo Septemba pili. Mzozo huu kati ya Somalia na Ethipia ulizua wasiwasi mkubwa kuhusu uthabiti wa eneo la Pembe ya Afrika, huku nchi nyingi na mashirika ya kimataifa yakihimiza kuheshimiwa kwa mamlaka ya Somalia.

Ethiopia ilipoteza eneo la bahari baada ya Eritrea kujitenga na kujitangazia uhuru wake mnamo mwaka 1993 baada ya vita vilivyodumu miongo mitatu.

(Vyanzo: APE, AFPE)