Somalia yaapa kulinda mamlaka yake kwa njia za kisheria
2 Januari 2024Uamuzi huo ni baada ya hatua ya Ethiopia ya kusaini makubaliano yenye utata na jimbo linalojitawala la Somaliland.
Makubaliano hayo ya kushitukiza yaliyofikiwa Jumatatu yanaipa nafasi Ethiopia ya kuifikia Bahari ya Shamu.
Somalia imesema makubaliano hayo ni ukiukaji wa wazi wa uhuru wake na imeziomba jumuiya za kimataifa kusimama upande wake.
Makubaliano hayo ya Addis Ababa yalitangazwa siku chache baada ya serikali kuu ya Somalia kukubali kufufua mazungumzo na jimbo la Somaliland linalotaka kujitenga, baada ya miaka kadhaa ya mkwamo.
Somaliland imekuwa ikitafuta kuwa nchi kamili tangu ijipatie uhuru wake kutoka Somalia mwaka 1991. Lakini harakati hizo zinapingwa vikali na serikali ya mjini Mogadishu na pia jimbo hilo la Somaliland halitambuliwi kimataifa.