1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSomalia

Somalia yahimiza ushirikiano wa kuwatokomeza Al Shabaab

Naomi Williams13 Januari 2023

Rais Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia ametoa wito kwa raia wa kawaida kushirikiana na kusaidia kuwaondoa wapiganaji wa kundi la Al-Shabaab aliowaita kunguni.

Somalia Mogadishu | Al-Shabaab Kämpfer während Militärübung
Picha: Farah Abdi Warsameh/AP/picture alliance

Akihutubia umati mkubwa wa watu katika mkutano ulioandaliwa na serikali dhidi ya wanamgambo hao wenye mafungamano na kundi la kigaidi la Al-Qaeda katika uwanja wa michezo mjini Mogadishu chini ya ulinzi mkali hapo jana, Rais Mohamud alisema ni wajibu wa kila raia kushiriki mapambano dhidi ya kundi hilo.

"Leo ninataka kuwaahidi kuwa tutafanya kazi pamoja ili kuwatokomeza na kuwaondoa Al-Shabaab kwa sababu ni kunguni ndani ya nguo zetu, lazima tuwaondoe  na kuwatokomeza hivi karibuni." Alisema Rais Mohamud

Wanamgambo wa al-Shabaab wamekuwa wakiendesha uasi wa umwagaji damu dhidi ya serikali dhaifu ya Somalia inayoungwa mkono na jumuiya ya kimataifa  kwa zaidi ya miaka 15. Kundi hilo limekuwa likifanya mashambulizi nchini Somalia na nchi jirani ambazo zilituma wanajeshi kusaidia katika mapambano dhidi ya wanamgambo hao. Rais Mohamud amesema wananchi wa Somalia wanaweza kushiriki vita dhidi ya Al-Shabaab kwa njia mbalimbali.

Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud Picha: Farah Abdi Warsameh/AP/picture alliance

Ameongeza kuwa Ukiona mtu usiyemjua karibu yako, ni vyema ukamuuliza ametokea wapi au kujitambulisha, na ukishindwa kufanya hivyo basi ni vyema ukapiga simu na kuripotimtu asiyejulikana katika eneo lako.

Rais huyo wa Somalia, alitangaza vita dhidi ya wapiganaji hao wanaofuata itikadi yao wenyewe ya Uislamu muda mfupi baada ya kuingia madarakani Mei mwaka jana. Katika miezi ya hivi karibuni, jeshi na wanamgambo wa koo wamechukua tena maeneo mengi katikati mwa nchi katika operesheni inayoungwa mkono na mashambulizi ya anga ya Marekani na kikosi cha Umoja wa Afrika.

Arish Yarisow mmoja wa waliohudhuria katika mkutano huo uliofanyika mjini Mogadishu amewatia shime wanaume kwa wanawake kuwa ni wakati sasa wa kulitokomeza kundi la Al Shabaab.

Soma :Jeshi la Somalia lawaua wapiganaji 20 Al Shabaab

"Kaulimbiu ya mkutano wa leo ni  ya kwetu sisi, wanaume na wanawake tujitokeze kupaza sauti, hatutaki damu yetu imwagike chini bila maana yoyote. Pia sisi  tunataka Al-Shabaab itokomezwe nchini baada ya miaka 15 ya changamoto na matatizo,"alisema Arish Yarisow aliyehudhuria mkutano huo.

Lakini waasi hao mara kwa mara wamekuwa wakilipiza kisasi kwa mashambulizi ya umwagaji damu, wakisisitiza uwezo wao wa kushambulia katikati ya miji na mitambo ya kijeshi ya Somalia.

Ingawa Al-Shabaab  walilazimishwa kuondoka katika mji wa  Mogadishu na vituo vingine vya mijini kwa zaidi ya muongo mmoja uliopita, lakini bado wamejikita katika maeneo ya vijijini katikati na kusini mwa Somalia.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW