Somalia yakabiliwa na hatari mpya ya njaa
21 Agosti 2026
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa WFP, Carl Skau, amesema shirika hilo kwa sasa lina rasilimali chache mno kulinganisha na kiwango cha fedha kilichokuwepo mwaka 2022, wakati lilipoongoza juhudi zilizosaidia kuzuia baa la njaa nchini Somalia.
Akizungumza wakati wa ziara katika kituo cha afya karibu na mji mkuu Mogadishu, Skau alisema WFP inalazimika kuweka kipaumbele kwa watoto wanaokabiliwa na utapiamlo mkali huku ikishindwa kuwafikia familia nyingi zinazohitaji msaada.
Kwa mujibu wake, uhaba wa fedha umezuia shirika hilo kuongeza misaada ya chakula kwa kaya zinazokabiliwa na njaa, pamoja na kuwasaidia akina mama wanaolea watoto walioathirika na utapiamlo.
Wafadhili wapunguza misaada
Skau amesema upungufu huo unatokana na nchi na taasisi nyingi za wafadhili kuelekeza fedha zao katika migogoro mingine ya kibinadamu duniani, hali iliyoacha shughuli za misaada nchini Somalia zikikabiliwa na ukosefu mkubwa wa rasilimali.
Ameonya kuwa tofauti kati ya mahitaji ya sasa na uwezo wa WFP ni kubwa mno, akieleza kwamba mwaka 2022 shirika hilo lilikuwa na rasilimali mara kumi zaidi ya lilizonazo sasa.
Katika mji wa Burhakaba, wanawake wengi wameripoti kulazimika kutembea kwa saa kadhaa kufika katika vituo vya afya kutokana na uhaba wa huduma karibu na maeneo wanayoishi.
Mmoja wao ni Halima Mohamed Hassan, mama wa watoto sita anayetarajia mtoto mwingine. Hassan alitembea karibu kilomita tatu akiwa amembeba mwanawe mwenye umri wa miaka minne anayesumbuliwa na utapiamlo. Amesema alikuwa hajapata chakula kwa siku mbili kabla ya kufika kituoni, huku mlo wake wa mwisho ukiwa wali pekee.
Ingawa watoto wake wengine pia wanakabiliwa na utapiamlo, amesema umbali wa safari na changamoto za usafiri zimemzuia kuwapeleka wote kupata matibabu.
Onyo la kuzorota kwa hali ya kibinadamu
WFP inakadiria kwamba watoto milioni 1.9 walio chini ya umri wa miaka mitano nchini Somalia wataathiriwa na utapiamlo mkali mwaka huu, huku karibu watoto laki tano wakihitaji matibabu ya haraka ya kuokoa maisha.
Umoja wa Mataifa umeonya kuwa karibu asilimia 30 ya wakazi wa Somalia wanakabiliwa na viwango vya kutisha vya ukosefu wa chakula. Mashirika ya misaada sasa yanazitaka serikali na wafadhili wa kimataifa kuongeza ufadhili haraka ili kuzuia mgogoro huo kugeuka kuwa janga kubwa la kibinadamu.