Somalia yaomba wanajeshi zaidi
15 Septemba 2011Waziri Mkuu, Abdiweli Mohamed Ali, mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa Somalia na wajumbe waandamizi wa Afrika katika Umoja wa Mataifa wote wametowa wito wa kutolewa kwa rasimali zaidi za kijeshi ili kuleta usalama katika mji mkuu wa Mogadishu ambapo mamia kwa maelfu ya watu wamekimbilia kutokana na maafa ya ukame ambayo tayari yameuwa maelfu ya watu.
Vikosi vya wanajeshi 9,000 kutoka Uganda na Burundi wanaunda kikosi cha Umoja wa Afrika ambacho kinailinda serikali ya mpito dhidi ya waasi wa al Shabab ambao hivi karibuni waliyatelekeza maeneo yao mjini Mogadishu.
Chini ya mamlaka iliyopewa na Umoja wa Mataifa kikosi hicho kinaweza kuwa na wanajeshi hadi 12,000 na Umoja wa Afrika umekuwa ukizidi kutowa wito wa kuongezwa kwa wanajeshi zaidi na kuruhusu kikosi hicho kuwa na wanajeshi 20,000 nchini Somalia.
Waziri Mkuu wa Somalia ameuambia mdahalo wa Baraza la Usalama kuhusu Somalia kwamba wanajeshi 3,000 zaidi wanahitajika kutumwa kwa haraka kuzuia kuwepo kwa ombwe la usalama katika maeneo yaliyotelekezwa na kundi la Shebab.
Ujumbe kama huo umetolewa na mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa Somalia Augustine Mahiga ambaye ameonya kwamba wababe wa vita wa Somalia wako tayari kuyachukua maeneo yaliyoachwa na al Shabab. Amesema wanamgambo wa siasa kali yumkini wakatumia mbinu za kigaidi mjini Mogadishu na kwengineko.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ametoa wito wa kuwekwa kwa kikosi maalum cha ulinzi mjini Mogadishu kuwalinda maafisa wa Umoja wa Mataifa na wafanyakazi wa kiraia wanaohudumia kikosi hicho cha kimataifa.
Mjumbe wa Afrika Kusini katika Umoja wa Mataifa Baso Sangqu ameelezea madai ya Umoja wa Afrika ya kutolewa kwa msaada mkubwa wa Umoja wa Mataifa kwa kikosi chao cha kijeshi kuzuia kuharibu mafanikio ya usalama ambayo yamepatikana.
Serikali dhaifu ya mpito imepewa miezi 12 mengine hadi mwezi wa Agosti mwaka 2012 kufikia malengo ya kuunda serikali na kuanzisha mazungumzo ya kisiasa ya taifa.
Balozi wa Uigereza katika Umoja wa Mataifa Mak Lyall Grant amesema msaada wa Baraza la Usalama kwa serikali ya Somalia unapaswa uwe na masharti kwa serikali ya mpito kutimiza malengo hayo.
Balozi huyo amesema wanataraji taasisi za serikali hiyo ya mpito kuonyesha uwajibikaji ulioboreka na uwazi hususan katika suala la utowaji na usimamizi wa raslimali pamoja na kuwa kitu kimoja na kujiepusha mizozo mingine zaidi ya ndani.
Viongozi wa Somalia wamekubaliana kuanza kutekeleza mpango ambao utamaliza kipindi kirefu cha mpito wa kisiasa ndani ya serikali nchini humo katika muda usiozidi miezi 12.
Mpango huo ulioidhinishwa wiki iliopita mjini Mogadishu na kamati ya serikali unataka kuboreshwa kwa usalama, kurasimu katiba na kufanyika kwa mazungumzo kuhusu usuluhishi wa kitaifa na utawala bora.
Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP, DPA
Mhariri: Josephat Charo