Somalia yataka vikosi vya ATMIS kutoondoka haraka
20 Juni 2024Kikosi hicho cha mpito cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia, ATMIS, kinatarajiwa kujiondoa kikamilifu nchini humo ifikapo Desemba 31, 2024, huku nafasi hiyo ikichukuliwa na kikosi kidogo zaidi.
Hata hivyo, serikali ya Mogadishu mwezi uliopita ilimwandikia barua kaimu mwenyekiti wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika na kuomba kucheleweshwa hadi mwezi Septemba, mchakato wa kuwaondoa nusu ya askari 4,000 waliopangiwa kuondoka Somalia mwishoni mwa mwezi Juni.
Awali, serikali ya Somalia ilipendekeza kwamba ratiba ya kuviondoa vikosi hivyo ni lazima irekebishwe kwa kuzingatia uhalisia, utayari na uwezo wa vikosi vya Somalia. Tathmini ya pamoja ya Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa, ilionya kwamba kuondolewa kwa haraka kwa kikosi cha ATMIS kutachangia uwepo wa ombwe la usalama.
Soma pia: ATMIS yakamilisha awamu mpya ya kuondoka Somalia
Kulingana na vyanzo vya kidiplomasia, Umoja wa Ulaya na Marekani ambao ndio wafadhili wakuu wa vikosi vya Umoja wa Afrika nchini Somalia, wamechukua uamuzi wa kupunguza idadi ya vikosi vya kulinda amani kutokana na wasiwasi wa kupatikana ufadhili wa muda mrefu. Mursal Khalif, mwanachama huru wa kamati ya ulinzi katika Bunge la Somalia amesema hali hii inamtia wasiwasi mkubwa hasa kuhusu mwelekeo wa taifa lake.
Vyanzo hivyo vimeendelea kueleza kuwa mazungumzo ya kuundwa kwa kikosi kipya yalikuwa na vuta nikuvute, Umoja wa Afrika ulishinikiza kupewa mamlaka yenye nguvu zaidi kuliko ilivyotakiwa na Somalia. Mzozo huu mkali wa kisiasa unaweza kusababisha Ethiopia kuwaondoa wanajeshi wake wanaosifiwa kwa umahiri. Ikulu ya Somalia na hata ofisi ya Waziri Mkuu hawakupendelea kuzungumzia mkasa huu.
Soma pia: Wasiwasi watanda Somalia kuondoka kwa kikosi cha Umoja wa Afrika
Mwakilishi maalum wa Umoja wa Afrika nchini Somalia na mkuu wa ATMIS, Mohamed El-Amine Souef amesema hapakuwa na muda mahsusi wa kuhitimisha mazungumzo hayo na kwamba pande zote zimefikia makubaliano yatakayosaidia kupatikana amani na usalama endelevu kwa kuhakikisha mchakato wa kuwaondoa askari wa kulinda amani unafanyika kwa hatua.
Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika linatarajiwa kukutana na kujadili hatima ya kikosi hicho.
Mchakato wa kujiondoa kwa kikosi hicho unaendelea
Tayari askari 5,000 kati ya 18,500 tayari waliondoka Somalia mwaka jana. Serikali ina matumaini na kikosi kipya kitakachochukua nafasi ya ATMIS na ambacho hakitozidi askari 10,000 na ambao watakuwa na jukumu la kulinda maeneo ya umma yenye mikusanyiko mikubwa ya watu.
Mchambuzi kwenye Taasisi ya utafiti yenye makao yake makuu mjini Nairobi ya Sahan, Rashid Abdi, anasema msukumo huu wa kuwepo kikosi kidogo nchini Somalia, unaakisi misimamo ya wale wanaojiita wazalendo na wanaopinga uwepo mkubwa wa vikosi vya kigeni nchini Somalia.
Soma pia:Al-Shabaab yashambulia kambi za jeshi Somalia na kuwaua watu 25
Uganda na Kenya, ambazo zilichangia wanajeshi katika kikosi hicho ambao pia wanatakiwa kuondoka nazo zina wasiwasi mkubwa kuhusu mustakabali wa Somalia. Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda Henry Okello Oryem, anasema licha ya juhudi kubwa za mafunzo kwa vikosi vya Somalia, askari wa nchi hiyo hawatoweza kuendeleza mapambano ya muda mrefu ya kukabiliana na magaidi wa al-Shabab.
Mwezi uliopita, Rais wa Kenya William Ruto aliwaambia waandishi habari mjini Washington, Marekani kwamba mchakato wa kukiondoa kikosi cha ATMIS bila kuzingatia hali halisi, hii itamaanisha kwamba magaidi hao wenye mafungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda wanaweza kuchukua madaraka nchini Somalia.
(Chanzo: RTRE)