Somalia yavunja masharti ya vikwazo vya silaha
13 Februari 2014Kwa mujibu wa ripoti ya siri iliyoandaliwa na Timu ya Waangalizi wa Umoja wa Mataifa kwa Somalia na Eritrea na kuwasilishwa kwa Kamati ya Vikwazo ya Baraza la Usalama, serikali ya Somalia inaruhusu kukiukwa kwa masharti kadhaa ya Baraza hilo na hivyo imeshauri ama marufuku hiyo ya silaha irejeshwe upya au angalau kuwekwe masharti ya kutolewa kwa taarifa za mara kwa mara juu ya silaha zinazoingia kwenye nchi hiyo iliyosambaratishwa kwa vita vya zaidi ya miongo miwili sasa.
Imegundulika kwamba serikali ya Somalia inagawa silaha kwa wanamgambo wa koo ambao si sehemu ya vyombo vya usalama. Miongoni mwao ni wale wa ukoo wa Abgaal wa Rais Hassan Sheikh Mohamed, ambaye mwezi uliopita aliliomba Baraza la Usalama kuongeza muda wa kulegezwa kwa marufuku hiyo, ambao unamalizika mwezi Machi.
"Mshauri mmoja mkuu wa rais kutoka ukoo wake wa Abgaal, amekuwa akihusika na mipango ya kufikisha silaha kwa kiongozi wa al-Shabaab aitwaye Sheikh Yussuf Isse, ambaye pia ni wa ukoo wa Abgaal." Inasema sehemu ya ripoti hiyo.
Mwezi uliopita, Rais Mohamud aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba serikali yake imekuwa ikifuata masharti yote ya Baraza la Usalama na kwamba alikuwa ameteua kamati maalum kuhakikisha hilo linafanyika.
Lakini ripoti hiyo ya inasema kuna ushahidi wa uhakika wa kuingizwa silaha zisizotambulika kwa njia ya ndege kutokea taifa moja la Ghuba mnamo mwezi Oktoba 2013 na kwamba baadhi ya silaha hizo zilihamishiwa kwenye eneo la faragha mjini Mogadishu.
Uamuzi wa Baraza za Usalama wa mwezi Machi 2013 kulegeza vikwazo vya silaha dhidi ya Somalia vilivyowekwa mwaka 1992, uliungwa mkono na Marekani kwa hoja ya kuisaidia serikali mpya ya Somalia kukabiliana na wanamgambo wa al-Shabaab.
Marufuku ya al-Shabaab juu ya intaneti yaingia Mogadishu
Wakati hayo yakiarifiwa, amri ya kupiga marufuku matumizi ya huduma za intaneti kupitia simu za mikononi iliyotolewa na al-Shabaab mwezi uliopita, sasa imeanza kutekelezwa hata kwenye mji mkuu Mogadishu, ambao uko kwenye mikono ya serikali.
Mwanzoni marufuku hiyo iliyoanza kutekelezwa tarehe 21 Januari ilikuwa inahusu maeneo ya kati na kusini pekee yanayoshikiliwa na al-Shabaab, lakini kisha ikasambaa hadi kwenye mikoa ya Hiran na Jubba ya Kati na Chini.
Kuanzia wiki iliyopita, ikiwa ni chini ya wiki moja baada ya al-Shabaab kuvamia ofisi za kampuni ya simu Hormuud Telecom mjini Jilib, kampuni hiyo imeacha kutoa huduma ya intaneti hadi kwenye maeneo yaliyo kwenye mikono ya serikali, ikiwemo Marka, Baidoa, Kismayu na Mogadishu.
Bado serikali ya Somalia haijasema chochote kuhusiana na kutanuka kwa marufuku hiyo ya al-Shabaab hadi mjini Mogadishu yaliko makao makuu ya serikali.
Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/dpa
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman