Somaliland yafungua ubalozi wake Jerusalem
16 Juni 2026
Katika sherehe za ufunguzi wa ubalozi huo zilizofanyika Jumatatu, Rais wa taifa hilo la Afrika Mashariki, Abdirahman Mohamed Abdullahi, alisema hiyo ni heshima kubwa, na hatua muhimu sana kwake kuifungua ofisi ya kwanza ya kidiplomasia ya Somaliland.
Rais Abdullahi ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X kwamba hatua hiyo ya kihistoria inaonyesha uwepo unaokua wa Somaliland kimataifa na ushirikiano unaoimarika kati ya Somaliland na Israel ambao umeanzishwa kwa heshima ya pande zote mbili.
Sherehe za ufunguzi wa ubalozi huo zilihudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Gideon Saar.
Hatua ya Somaliland yakosolewa vikali
Siku ya Jumatatu, Jumuiya ya Ushirikiano wa Nchi za Kiislamu OIC, ililaani vikali hatua ya Somaliland kuufungua ubalozi wake mjini Jerusalem na kuthibitisha tena kuendelea kuunga mkono uhuru na mamlaka ya Somalia.
OIC, yenye nchi wanachama 57 imeitolea wito jumuia ya kimataifa kuchukua hatua kali dhidi ya kitendo hicho walichosema ni kinyume na sheria.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina, pia imelaani vikali hatua ya Somaliland kuufungua ubalozi wake mjini Jerusalem.
Abdullahi ameufungua ubalozi huo ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku tano nchini Israel iliyoanza Juni 14. Siku ya Jumapili, rais huyo wa Somaliland alikutana na Rais wa Israel, Isaac Herzog, na kusema kuwa ziara hiyo ina umuhimu mkubwa sana.
''Hii ni ziara ya kwanza kufanywa na Rais wa Jamhuri ya Somaliland kwenye nchi nyingine, na tunashukuru kwamba taifa la Israel limechagua kutupokea kwa heshima kubwa katika tukio hili la kihistoria. Kwa kufanya hivyo, Israel imeshiriki katika wakati ambao utakumbukwa katika historia ya kidiplomasia ya taifa letu, na tunaichukulia hali kwa uzito mkubwa,'' alisisitiza Abdullahi.
Somaliland ilijitangazia uhuru wake kutoka kwa Somalia mnamo mwaka 1991, lakini kwa muda mrefu haijawahi kutambuliwa kimataifa. Mwezi Desemba mwaka 2025, Israel ilikuwa nchi ya kwanza kutangaza kuitambua rasmi Somaliland kama taifa huru.
Nchi nane zina balozi zake Jerusalem
Nchi kadhaa katika eneo hilo zililaani vikali hatua hiyo. Nayo serikali ya Somalia imeendelea kupinga vikali hatua ya Israel kuitambua Somaliland.
Somaliland ni nchi ya nane kufungua ubalozi wake mjini Jerusalem, baada ya Marekani, Guatemala, Honduras, Kosovo, Papua New Guinea, Paraguay na Fiji ambazo pia balozi zake ziko Jerusalem.
Balozi nyingi za kimataifa nchini Israel ziko Tel Aviv, kutokana na hadhi ya Jerusalem kuwa moja ya masuala tete zaidi kati ya Israel na Palestina.