Afrika Kusini yaishutumu Israel uhalifu wa kivita
21 Novemba 2023Shtuma hizo amezitoa wakati alipokuwa akiongoza mkutano wa kilele wa kundi la mataifa ya BRICS ili kujadili mzozo kati ya Israel na kundi la Hamas. Ramaphosa amesema adhabu ya jumla ya raia wa Palestina inayoendeshwa na Israel kwa kutumia nguvu kinyume cha sheria, ni uhalifu wa kivita, na kwamba kuzuia kwa makusudi usambazaji wa dawa, mafuta, chakula na maji kwa wakazi wa Gaza ni sawa na mauaji ya halaiki.Mkutano huo umehudhuriwa kwa njia ya mtandao na viongozi mbalimbali akiwemo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, Rais wa Urusi Vladimir Putin pamoja na viongozi kutoka mataifa ya Saudi Arabia, Argentina, Misri, Ethiopia, Iran na Umoja wa Falme za Kiarabu, ambao wanatazamiwa pia kujiunga na jumuiya hiyo.Kwa sasa BRICS inazijumuisha Brazil, Urusi, India, China na Afrika Kusini, na ni kundi la mataifa makubwa yanayoinukia kiuchumi yanayolenga kuunda utaratibu mpya wa kimataifa unaokinzana na ule unaoongozwa na Marekani na mataifa ya Magharibi.