1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

SPD yataka kujadili upya baadhi ya masuala na CDU/CSU

22 Januari 2018

Kiongozi wa chama cha SPD Martin Schulz amesema anataka kujadili upya masuala muhimu ambayo awali yalikuwa yameshajadiliwa kati ya chama chake na vyama ndugu vya kihafidhina vya CDU na CSU.

Deutschland Abschluss der Sondierungen von Union und SPD
Picha: picture-alliance/Photoshot/S. Yuqi

Kiongozi wa chama cha SPD Martin Schulz ametoa ahadi hiyo ya kurejea masuala muhimu katika mazungumzo ya kuunda serikali ya muungano. Msimamo wake huo mgumu unafuatia kuungwa mkono kwa wingi mdogo na chama chake kwa ajili ya mazungumzo hayo. Bwana Schulz amesema atakutana baadae na kiongozi wa chama CDU kansela Angela Merkel na kiongozi wa chama ndugu cha CSU Horst Seehofer.

Kiongozi wa chama cha SPD Martin SchulzPicha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

Mwenyekiti wa SPD, Martin Schulz ametilia mkazo msimamo wa chama chake kwamba mada muhimu zinazohusu masilahi ya jamii zinajumuishwa katika mazungumzo kabla ya kufikia makubaliano ya mwisho. Wanachama cha SPD watatakiwa mwishoni mwa mazungumzo hayo yatakayopoanza leo usiku kutamka kama wanakubaliana kwa kauli moja kwamba serikali mpya iundwe au sivyo.

Hata hivyo Washirika wa kansela  Angela Merkel wanapinga mabadiliko yoyote kwenye makubaliano ambayo yalikuwa tayari yameshafikiwa katika mazungumzo ya mwanzo.

Katibu mkuu wa chama cha SPD Lars KlingbeilPicha: picture alliance/dpa/K. Nietfeld

Katibu Mkuu wa chama cha SPD Lars Klingbeil amewaambia waandishi wa habari wa shirika la ARD la hapa nchini Ujerumani kwamba chama chake kinataka kuongeza kipendgele cha "shida" katika makubaliano juu ya uhamiaji ambayo yatazingatia idadi ya wakimbizi 1,000 kwa mwezi ambao wanaweza kujiunga kwenye kambi za wakimbizi waliokubaliwa nchini Ujerumani chini ya sheria ya kujumuika pamoja kwa familia.

Pia ana matumaini ya kufikia maelewano juu ya mifumo katika huduma ya afya ya umma na ile ya kibinafsi ambapo chama cha SPD kinataka ibadilishwe hatua ambayo vyama vya kihafidhina inaipinga.

Ikiwa viongozi wa SPD hawatoweza kutatua masuala hayo muhimu, hatari iliyopo ni kwamba wanachama wanaweza kukataa kuyapitisha makubaliano ya mwisho, ambayo kiongozi wa SPD Martin Schulz anapanga kupokea kura zote za ndio kutoka kwa wanachama wake 443,000.

Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: Reuters/F. Bensch

Kwa vyovyote vile kansela Angela Merkel anahitaji ushirikiano na SPD ili kuweza kuhudumu katika muhula wa nne ndiposa anakitaka chama cha SPD kikubali kurejea tena kwenye serikali la muungano baina ya vyama hivyo vya CDU/CSU pamoja na chama cha SPD na kuweza kuongoza kwa mara nyingine kama ilivyokuwa mnamo mwaka 2013 katika taifa lenye nguvu ya kiuchumi barani Ulaya.

 

Mwandishi: Zainab Aziz/RTRE

Mhariri: Iddi Ssessanga

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW