SPD yaunga mkono mazungumzo na Merkel
21 Januari 2018Hatua hiyo imeliingiza taifa hilo ambalo ni uchumi mkubwa katika bara la Ulaya hatua moja karibu na kupata serikali imara baada ya miezi kadhaa ya hali ya sintofahamu ya kisiasa.
Wajumbe wa chama cha SPD walipiga kura 362 za 'ndio' dhidi ya kura 279 za 'hapana" kusongambele na majadiliano baada ya viongozi wa chama hicho cha siasa za wastani zan mrengo wa kushoto kukubali muongozo wa muungano pamoja na kundi la vyama vya kihafidhina vinavyoongowa na kansela Merkel mapema mwezi huu. Hakuna mjumbe aliyejizuwia kupiga kura.
Mazungumzo yanatarajiwa kuanza wiki hii, na kuleta ahueni kwa washirika wa Ujerumani barani Ulaya , ambako Merkel kwa muda mrefu amechukua nafasi ya uongozi katika masuala ya kiuchumi na usalama. Wajumbe wa chama cha SPD bado watakuwa na nafasi ya kupiga kura katika makubaliano ya mwisho ya kuunda serikali , kama yatapatikana.
Kiongozi wa chama cha Social Democratic SPD Martin Schultz hapo awali katika hotuba yake kwa wajumbe aliwataka wanachama wa chama hicho kupiga kura kwa ajili ya kufungua mazungumzo ya kuunda serikali ya mseto na chama cha kansela Merkel, akisema serikali imara ya Ujerumani inahitajika kuimarisha Ulaya na kuwa kama ukuta dhidi ya siasa kali za mrengo wa kulia.
Uamuzi wake ulikuwa sahihi
Chama hicho cha siasa za wastani za mrengo wa kushoto kimeshiriki katika serikali na kundi la vyama vya kihafidhina la kansela Angela Merkel tangu mwaka 2013, lakini Schultz aliapa kutorejea tena katika kile kinachoitwa "muungano mkuu" baada ya chama chake cha Social Democratic kupata kipigo katika uchaguzi wa mwezi Septemba.
Amewaambia wanachama wa chama chake waliokusanyika mjini Bonn kwamba uamuzi wake ulikuwa sahihi katika wakati ule, lakini alisema hali ya kisiasa imebadilika baada ya Merkel kushindwa kuunda serikali pamoja na vyama viwili vidogo.
"Ulaya inaisubiri Ujerumani ambayo inafahamu wajibu wake kwa ajili ya Umoja wa Ulaya na inaweza kuchukua hatua muafaka," alisema.
Amesema hali ni ngumu, wakati rais wa Ufaransa Emmanuel Macron anahitaji kuungwa mkono kwa mipango yake ya kuufanyia mageuzi Umoja wa Ulaya.
"Iwapo atashindwa katika sera zake , haitawezekna kuondoa uwezekano wa makundi yenye siasa kali za mrengo wa kulia kuunda serikali ijayo mjini Paris," Schutz alisema.
Iwapo Wasocial Democrats watakataa kuingia katika mazungumzo , fursa pekee iliyokuwa imebaki ni kwa Merkel kuunda serikali yenye wingi mdogo ama kuitisha uchaguzi mpya.
Naibu kiongozi wa chama cha Social Democratic Malu Dreyer , gavana wa jimbo la Rhineland-Palatinate, aliwaambia wajumbe wa mkutano huo kwamba kwa kuwa kundi la vyama vinavyoongozwa na Merkel linapinga kuunda serikali yenye wingi mdogo , kupiga kura dhidi ya kuingia katika mazungumzo hayo kutakuwa na maana ya kufanyika uchaguzi mpya.
Vijana wanapinga makubaliano hayo
"Hatuwezi kuvilazimisha vyama vya kihafidhina kuunda serikali ya wingi mdogo, hii ni kitu ambacho hakipo," alisema.
Lakini kiongozi wa tawi la vijana la chama cha Social Democratic , Kevin Kuehnert, aliwahimiza wajumbe kupiga kura dhidi ya kuingia katika muungano huo wa serikali, akisema kukubali kwa sababu tu ndio njia pekee iliyobakia kutachangia zaidi katika matatizo makubwa ya chama hicho ya kutoaminika na waungaji wake mkono.
"Mzunguko huu ni lazima uvunjwe," amesema Kuehnert , ambaye aliongoza upinzani mkali dhidi ya kuingia katika mazungumzo mapya ya kuunda serikali ya muungano.
Wengi wa wanachama wa chama cha Social Democratic wameeleza hofu yao kwamba watakapoingia katika muungano wa serikali mpya , hii itakiweka chama kinachopinga wahamiaji cha Alternative for Germany , chama mbadala kwa Ujerumani AfD kuwa chama kikuu cha upinzani bungeni.
Lakini Schulz amesema kitisho cha uchaguzi mpya ni kikubwa zaidi. "Nani anaweza kusema kwamba uchaguzi mpya hautaimarisha zaidi kundi la siasa kali za mrengo wa kulia?" aliuliza.
Alidokeza kwamba Wa Social Democrats wengine barani Ulaya hawajafidika na kuwa katika nafasi hiyo, na kueleza kwamba nafasi nzuri kwa chama chake kupata kuungwa mkono zaidi kutoka mashinani ni kupitia kuendeleza kwa nguvu zote sera zake kutokea ndani ya serikali na kuchukua hatua kama chama mshirika mdogo na Merkel.
"Serikali yoyote ambacho chama cha SPD kitashiriki , bila kujali ni muungano gani, inapaswa kuwa serikali ya SPD," alisema. "Huo ni lazima uwe msimamo wetu."
Mwandishi : Sekione Kitojo / ape
Mhariri: Isacc Gamba