Spika mstaafu wa Tanzania Job Ndugai aaga dunia
6 Agosti 2025
Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Kongwa Job Ndugai, amefariki dunia leo Agosti 6, 2025, huko jijini Dodoma ambako alikuwa akipatiwa matibabu baada ya kuugua ghafla.
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani, Dkt. Tulia Ackson amethibitisha kifo cha Ndugai na kuelezea masikitiko makubwa.Job Ndugai amuomba radhi rais Samia na Watanzania
“Kwa masikitiko makubwa, naomba kutoa taarifa ya kifo cha kiongozi wetu, mwanasiasa mkongwe na Spika Mstaafu wa Bunge Mheshimiwa Job Yustino Ndugai kilichotokea leo jijini Dodoma. Natoa pole kwa familia ya Marehemu, ndugu, jamaa na Wananchi wa Jimbo la Kongwa, Mwenyezi Mungu awape moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu,” amesema Spika Tulia.
Aidha ofisi ya Bunge kwa kushirikiana na Kamati ya Mazishi pamoja na familia ya Marehemu imeeleza kuwa inaratibu mipango ya mazishi na taarifa zaidi zitaendelea kutolewa.
Marehemu Ndugai alizaliwa tarehe 22 Januari 1963 na amekuwa Spika wa Bunge kuanzia mwaka 2015 hadi 2022, kabla ya kujiuzulu.
Mwaka huu alishinda tena kura za maoni ambapo alitia nia ya kutetea kiti chake kama Mbunge wa jimbo la Kongwa kupitia chama tawala CCM.