1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Spika Pelosi aizuru Taiwan licha ya onyo la China

3 Agosti 2022

Licha ya vitisho kutoka Beijing, Spika wa Baraza la Wawakilishi la Marekani, Nancy Pelosi, amewasili Taiwan na kuzungumza na rais na naibu spika wa bunge, huku China ikifanya mazoezi ya kijeshi karibu na kisiwa hicho.

Taiwan Nancy Pelosi und Präsidentin Tsai Ing-wen
Picha: Taiwan Pool via REUTERS

Mwanasiasa huyo wa Kimarekani mwenye umri wa miaka 82 aliwasili mjini Taipei na ujumbe wake usiku wa Jumanne (Agosti 2), akikaidi maonyo na vitisho vikali vilivyotolewa na China, ambayo inaitambuwa Taiwan kuwa ni mamlaka yake na tayari ilishatangaza kuwa ingeliichukulia ziara ya Pelosi kuwa ni uchokozi mkubwa na wa wazi dhidi yake.

Akizungumza na naibu spika wa bunge la Taiwan, Tsai Chi-chang, mara baada ya kuwasili, Pelosi alihalalisha ziara yake kwenye kisiwa hicho kwamba haivunji makubaliano yoyote kati ya China na Marekani na kwamba lengo lake kuu ni kuonesha uungaji mkono wake kwa demokrasia ya Taiwan.

"Lengo letu, au malengo yetu matatu niliyosema, katika kufanya hivi, tunataka kuongeza mashirikiano na majadiliano baina ya mabunge yetu. Na tunafanya hivyo wakati rais wetu amependekeza mpango wa uhusiano wa Asia na Pasifiki, ambao tunauunga mkono na tunataka tuwe makini kabisa juu ya namna tunavyoshirikiana na Taiwan kwenye jambo hili." Alisema Pelosi.

Rais Tsai Ing-wen wa Taiwan (kulia) akimkaribisa Spika wa Baraza la Wawakilishi la Marekani, Nancy Pelosi, mjini Taipei.Picha: Taiwan Pool via REUTERS

Baadaye akiwa na Rais Tsai Ing-wen, spika huyo wa bunge la Marekani alisema yeye na wenzake wamekwenda Taiwan na "ujumbe wa urafiki na amani kwenye eneo lote."

Wasiwasi watanda

Kwa upande wake, Rais Tsai Ing-wen wa Taiwan amesema kisiwa hicho hakitayumbisha na vitisho vya China ambayo imeamuwa kufanya mazoezi ya kijeshi karibu sana na kisiwa chao wakati huu wa ziara ya Spika Pelosi.

"Japo tunakabiliwa na vitisho vya hali ya juu vya kijeshi, Taiwan haitarudi nyuma. Tutaendelea na kushikilia uzi huu huu kwa ajili ya kuilinda demokrasia." Alisema rais huyo.

Pelosi, ambaye ni wa pili kwa madaraka nchini Marekani baada ya Rais, aliwasili akiwa kwenye ndege ya kijeshi baada ya siku kadhaa za uvumi juu ya mipango yake.

China yaapa kuchukuwa hatua

Spika Nancy Pelosi wa Marekani (katikati) akitembelea bunge la Taiwan siku ya Jumatano (Agosti 3, 2022).Picha: Ann Wang/REUTERS

Mara tu baada ya kuwasili kwake, China ilitangaza hatua za mara moja kuonesha upinzani wake, ikiwemo ya kumuita Balozi wa Marekani mjini Beijing, Nicholas Burns, ambaye ilimwambia wazi kwamba Washington italipia gharama ya hatua hiyo ya Pelosi.

Jeshi la China linafanya mazoezi ya kivita umbali wa kilomita 20 tu kutoka fukwe za Taiwan, likisema liko kwenye hali ya hadhari ya kiwango cha juu, tayari kuchukuwa hatua hatua yoyote kujibu uchokozi huo wa Marekani kama ikibidi.

Wizara ya ulinzi ya Taiwan nayo imeliweka jeshi lake katika hali ya hadhari, ingawa limetowa tamko la kuwataka raia waendelee na shughuli zao kama kawaida.

Wizara hiyo imesema kuwa zaidi ya ndege 21 za kijeshi za China zimeingia kwenye anga lake tangu jana usiku. 
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW