1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Spika Pelosi kumfungulia uchunguzi Trump

Yusra Buwayhid
25 Septemba 2019

Spika wa Bunge la Marekani Nancy Pelosi ametangaza kuanzisha uchunguzi rasmi wa kumfungulia mashtaka Rais Donald Trump. Ni hatua ya kwanza katika mchakato ambao unaweza kumuondoa rais huyo madarakani.

USA | Nancy Pelosi will Donald Trumps Amtsenthebung einleiten
Picha: Getty Images/A. Wong

Inadaiwa Trump alizungumza kwa simu na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky mnamo Julai 25, kumtaka msaada wa kumuangamiza mpinzani wake katika kampeni yake ijayo ya uchaguzi wa rais.

Trump inadaiwa alimshinikiza rais wa Ukraine kutafuta njia za kuchafua sifa ya makamu wa rais wa zamani Joe Biden na mtoto wake, Hunter. Kupitia tiketi ya chama cha Democratic, Biden anaweza kuwa mpinzani wa Trump katika uchaguzi ujao wa rais wa 2020.

Tangazo hilo lilitolewa baada ya mtu aliyekataa kutajwa kwa majina kuvujisha taarifa hizo za siri na kuwasilisha lalamiko kuhusu mazungumzo hayo ya simu ambapo rais Trump alimpigia mwenzake wa Ukrain rais Volodymyr Zelensky.

"Inasikitisha sana, kufikiria kwamba rais wetu anaweza kufanya kosa la kufunguliwa mashtaka. Ni ngumu, unajua? Ni ngumu kusema tumefika katika hali hiyo," amesema Pelosi akitoa taarifa hiyo kwa njia ya televisheni.

Trump asema mazungumzo yalikuwa ya kirafiki

Trump alikiri kwamba kwa muda mfupi alizuia fedha za msaada kwa Ukraine zipatazo dola milioni 400, lakini alikana kufanya hivyo kwa lengo la kumshinikiza Zelenskiy aanzishe uchunguzi ambao utaharibu sifa ya Biden. Pesa hizo za misaada hatimaye zilitolewa wiki iliyopita.

Rais Donald Trump akiwa katika Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa.Picha: picture-alliance/Photoshot

Trump pia ameidhinisha maandishi ya mazungumzo hayo ya simu yachapishwe, na yataweza kuonekana na umma Jumatano. Rais huyo wa Marekani amesema watu wataona kwamba yalikuwa ni mazungumzo ya kirafiki ambayo hayana kosa lolote.

Hata kama Baraza la Wawakilishi linalodhibitiwa na Wademocrat litapiga kura ya kumfungulia mashataka Trump, kuna uwezekano mdogo wa rais huyo kuondolewa madarakani. Wabunge wa chama cha Trump cha Republican watapinga katika baraza la seneti ambako uamuzi huo wa kumfanyia uchunguzi utahitaji thuluthi mbili za kura kupitishwa.

Lakini mchakato huo unaweza kuharibu sifa ya Trump akiwa anaelekea kugombea achaguliwe tena, huku asilimia 45 ya Wamarekani wakiukubali utendaji wake kama rais, hasa taarifa za kumchafulia jina zikitoka wakati akiwa ameshaanza mikutano ya kampeni.

Kwa upande mwengine mchakato huo pia unaweza kumsaidia Trump, iwapo Wamarekani wataamini kwamba chama cha Democratic kinamlenga kwa ubaya rais huyo.

Soma zaidi:Trump na spika wa Baraza la Wawakilishi wanazidi kuzozana

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW