Spika Uturuki ataka katiba ya Kiislamu
26 Aprili 2016Kwa mujimu wa video zilizochapishwa na vyombo vya habari nchini Uturuki, spika wa bunge Ismail Kahraman alisema katika hotuba siku ya Jumatatu, kwamba katiba mpya haipaswi kuwa ya kilimwengu.
"Inapaswa kujadili dini, haipaswi kuwa isiyo na dini, bali inapaswa kuwa katiba ya kidini," alisema Kahraman, ambaye katika nafasi yake ya uspika, anasimamia juhudi za kuandaa muswada wa katiba mpya.
Chama tawala cha Haki na Maendeleo AKP, ambacho kina misingi yake katika siasa za Kiislamu, kinashinikiza kubadilishwa kwa katiba ya sasa, ambayo iliandikwa baada ya mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 1980.
Hofu ya Erdogan kujilimbizia madaraka
Wakosoaji wanahofia kwamba katiba hiyo mpya huenda ikampa madaraka makubwa rais Racep Tayyip Erdogan, ambaye anataka mfumo urais weenye mamlaka zaidi uchukuwe nafasi ya mfumo wa sasa wa bunge. Serikali imeahidi kuwa viwango vya Ulaya kuhusu haki za binaadamu vitakuwa msingi wa maandishi ya katiba mpya.
Chama cha AKP kina viti 317 kati ya 550 vya ubunge na kitahitaji kura 330 kuwasilisha musada wa katiba kwa ajili ya kuupigia kura ya maoni, hii ikimaanisha kuwa laazima ipate uungwaji wa wabunge kutoka vyama vingine.
Kamal Kilicdaroglu, kiongozi wa chama kikuu cha upinzani na kisichofuata misingi ya dini cha Republican People'r Party CHP, aliadika katika ukurasa wake wa twitta akimjibu spika wa bunge kwamba: Kutoifanya dini kuwa msingi wa maadili ndiyo kanuni ya msingi ya amani ya kijamii...na kwamba hilo linahakikisha kuwa kila mtu ana uhuru wa dini.
Mwenyekiti ya tume ya katiba akanusha
Lakini mwenyekiti wa tume ya katiba Mustafa Sentop amesema leo kuwa katiba ya Uturuki itabakisha muongozo wake wa kilimwengu, na kwamba chama cha AKP hakijafanya majadiliano yoyote kuhusu kuuondoa muongozo huo.
Uturuki amabyo ni mwanachama wa jumuiya ya Kijihami NATO na inayotaka kujinga na Umoja wa Ulaya, imekuwa ikitolewa mfano kwa muda mrefu na washirika wake wa Magahribi kama ruwaza ya taifa lenye Waislamu wengi linalofuata muongozo wa kilimwengu na la kidemokrasia.
Kahramman alisema tayari katiba ya sasa ni ya kidini kwa sababu inazitambua siku kuu za kiislamu kuwa siku za mapumziko, hata kama inashindwa kumtaja "Allah" hata mara moja.
Uislamu uliondolewa kuwa dini rasmi 1924
Uturuki iliifanyia mabadiliko katiba yake ya awali ya mwaka 1924 miaka minne baadae na kuuondoa Uislamu kama dini rasmi ya taifa lililoasisiwa na Mustafa Kemal Ataturk. Wanahistoria wanaichukulia hatua hiyo kuwa ndiyo msingi wa jamhuri ya sasa ya kidemokrasia na kilimwengu ya Uturuki. Katiba ya sasa haitambui dini yoyote kuwa rasmi.
Kilicdaragou amesema migogoro inayoendelea katika maeneo mengi ya kanda ya Mashariki ya Kati inatokana mara nyingi na mizozo ya kidini, na kuonya dhidi ya matumizi mabaya ya dini. Spika Kahram aliwahi kuwa mwanachama wa chama cha Ustawi - Refah - kilichopigwa marufuku mwaka 1998 na mahakama ya katiba kwa kukiuka miongozo ya kilimwengu. Waanzilishi muhimu wa chama cha AKP, akiwemo rais Erdogan walikuwa wanachama wa Refah.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre,dpae
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman