1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUganda

Spika wa bunge la Uganda afariki dunia

Ibrahim Swaibu
20 Machi 2022

Spika wa bunge la Uganda Jacob Oulanyah amefariki dunia leo Jumapili akiwa nchini Marekani alikopelekwa kwa matibabu.

Uganda I Parlamentswahlen
Picha: Parliamentary Press Office/Uganda

Taarifa hizo zimetolewa na rais wa Uganda Yoweri Museveni kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Rais Museveni ameandika, "Wananchi wenzangu, kwa masikitiko makubwa ninatangaza kifo cha  Mheshimiwa Jacob Oulanyah, spika wa bunge.” huku akiongeza kwamba  alipokea taarifa za kifo chake nyakati za saa nne na nusu asubuhi kwa saa za Afrika Mashariki kutoka kwa watu waliokuwa karibu na marehemu katika chumba cha wagonjwa mahututi

Hata hivyo, katika ujumbe wake rais  Museveni hakubainisha chanzo cha kifo cha spika Oulanya.

Hata hivyo itakumbukwa mnamo Februari 3 2022, serikali ya Uganda ilikodesha ndege ya shirika lake la ndege Uganda Airlines kumpeleka spika huyo nchini Marekani kwa ajili ya matibabu baada ya kuugua kwa takriban siku saba nchini Uganda.

Wakati wa kufikiwa na mauti spika huyo amekuwa akiendelea kupokea matibabu katika jimbo la Seatle nchini Marekani.

Mnamo Machi 15 mwaka huu timu  ya maafisa kutoka Uganda ikiongozwa na naibu spika wa Uganda  Anita Among, kiongozi wa chama cha upinzani cha Democratic Party Nobert Mao, Hakimu Mkuu Owiny-Dollo pamoja na waziri wa afya Ruth Aceng walisafiri hadi nchini Marekani kumtembelea spika Oulanyah.

Baada ya ziara hiyo Nobert Mao alibainisha kuwa naibu spika Anita Among  angewaambia wananchi wa Uganda kuhusu hali ya afya ya spika lakini aliwataka Waganda kuzidi kumuombea afya nzuri.

Kifo chake kilitanguliwa na habari za uzushi mitandaoni

Picha: Parliamentary Press Office/Uganda

Wiki iliyopita, katika mitandao ya kijamii nchini humo kulizagaa taarifa kwamba Oulanya alikuwa amefariki, habari ambazo mkurugenzi wa mawasiliano bungeni Chris Obore alikanusha na kuzitaja kama habari za uongo.

Hata hivyo hakueleza hali ya afya ya Spika, lakini alisisitiza kwamba "Hata kama kuna tatizo, mtu sahihi wa kusema chochote ni Naibu Spika. Wacha tusubiri arudi, na tunaweza kumuuliza. Kwa sasa tuheshimu faragha ya Spika.”

Among amekuwa akiongoza bunge tangu Februari 3, wakati Oulanyah aliposafirishwa hadi Seattle nchini Marekani kwa matibabu maalumu.

Jacob Oulanyah ni nani?

Mwanachama wa Chama tawala cha NRM kinachoongozwa na rais Museveni, Jacob amekutwa na mauti wakati akiwa ndio spika wa bunge la 11 la nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Picha: Parliamentary Press Office/Uganda

Alichaguliwa katika wadhifa huo mnamo Mei 24 baada ya kumshinda Rebecca Kadaga katika kinyang'anyiro hicho.

Jacob L'Okori Oulanyah alizaliwa  Machi 23 1965 katika Wilaya ya Gulu  kaskazini mwa Uganda wakati huo.  Baada ya kukamilisha elimu yake ya sekondari, Jacob alijiunga na  cha Makerere mnamo mwaka 1988 ambapo alisomea uchumi wa kilimo. Alihitimu mnamo 1991 na Shahada ya Sanaa katika somo hilo.

 Mwaka huo huo, alianza safari mpya ya masomo yake akichaguwa  kusoma sheria na kuhitimu mwaka wa 1994 na shahada ya Sheria. Wakati  huo, alihudumu kama kama spika wa chama cha wanafunzi wa chuo kikuu.

Kabla ya kuchukua hatamu kama spika, Jacob alihudumu  pia kama naibu spika  wa Uganda chini ya mtangulizi wake Rebeca Kadaga kuanzia mwaka 2011 hadi 2021.

Hadi  kufikia sasa watu mbali mbali wakiwemo rais Museveni, aliyekuwa spika wa bunge Rebecca Kadaga,wanasiasa, wandishi habari pamoja na watu mbali mbali wanaendelea kutuma risala za rambi rambi kwa familia ya spika huyo.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW