1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Spika wa Tanzania achaguliwa kuwa rais wa Mabunge duniani

27 Oktoba 2023

Spika wa Bunge la Tanzania Tulia Ackson amechaguliwa kuwa raisi wa 31 wa Umoja wa Mabunge Duniani, IPU, katika kikao cha Baraza la Uongozi wa muungano huo kilichofanyika mjini Luanda, nchini Angola.

Dr. Tulia Ackson
Spika wa Bunge la Tanzania Tulia AcksonPicha: Ericky Boniphace

Katika kura ya siri iliyopigwa wabunge wapatao 700 kutoka mataifa 130 ikiwemo wajumbe kutoka mataifa yalioko vitani au katika mazingira ya mizozo, Spika Tulia Ackson amewashinda wagombea wengine watatu kwa kupata asilimia 57 ya kura katika duru ya kwanza y aupigaji kura.

Dr. Ackson anachukuwa nafasi hiyo kutoka kwa Duarte Pacheco, mbunge kutoka Ureno, ambaye amekamilisha muhula wake wa miaka mitatu katika mkutano wa 147 wa IPU.

Ili kuhimiza usawa wa kijinsia, kila bunge mwanachama wa IPU lilipewa kura tatu kwa sharti la kuwa na ujumbe wenye usawa wa kijinsia, huku ujumbe wenye jinsia moja tu ukipewa kura moja.

Na katika tukio la kwanza na la kihistoria katika uchaguzi wa safari hii, wagombea wengine watatu kwenye karatasi ya kura - Adji Diarra Mergane Kanoute kutoka Senegal, Catherine Gotani Hera wa Malawi na Marwa Abdibashir Hagi wa Somali walikuwa wote wanawake kutoka barani Afrika.

Soma pia:Spika azuia mjadala kuhusu mkataba wa bandari ya Tanzania

Dk. Ackson ndiye mwanamke wa tatu kuchaguliwa rais wa IPU, baada ya Najma Heptulla kutoka India, na Gabriela Cuevas kutoka Mexico. Pia ndiye mwanamke wa kwanza wa Afrika kushika wadhifa huo.

"Naikubali nafasi hii kwa unyenyekevu wote, huku nikitambua majukumu yanayoambatana nayo," alisema Dr. Ackson baada ya kutangazwa mshindi.

"Ninathibitisha tena dhamira yangu ya kufanya kazi pamoja nanyi nyote ili kuifanya IPU kuwa shirika lenye ufanisi zaidi, linalowajibika na lililo wazi," aliongeza.

Historia ya kisiasa ya Dr. Tulia Ackson

Ackson aliteuliwa kwa mara ya kwanza kuwa mbunge nchini Tanzania mwaka 2015, ambapo alikuwa naibu wa spika kabla ya kuchaguliwa kuwa spika kamili mwaka 2022. Pia aliwahi kuhudumu kama Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali mwaka 2015.

Tulia Ackson ashinda urais wa Umoja wa Mabunge Duniani IPU

01:25

This browser does not support the video element.

Ni msomi wa sheria aliehitimu na kutunukiwa shahada na shahada ya uzamili katika fani ya sheria kutoka chuo kikuu cha Dar es Salaam, na shahada ya uzamivu katika fani hiyo kutoka shuo kikuu cha Cape Town cha nchini Afrika Kusini.

Dr. Ackson ambaye pia ni Wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania na mwanachama wa Chama cha Wanasehria wa Tanganyika, TLS, alikuwa mhadhiri katika kitivo cha sheria cha chuo kikuu cha Dar es Salaam.

Soma pia:Spika wa Tanzania asema matukio ya mauaji yasitangazwe

Baraza la Uongozi la IPU humchagua rais wake kwa muhula wa miaka mitatu, akiwa mkuu wa kisiasa wa muungano huo anaeongoza vikao vya kisheria na kuwakilisha shirika hilo katika matukio ya kimataifa.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kuptia Ukurasa wake wa mtandao wa Kijamii wa X, zamani Twitter, amempongeza Spika Tulia, akisema ushindi wake ni ushuhuda wa kazi kubwa anayoendelea kuifanya, na imani walionayo wajumbe juu yake na nchi ya Tanzania.

Ujumbe wa kumpongeza Dr. Tulia umehanikiza kwenye mitandao ya kijamiilakini pia wakosoaji wanaosema kiongozi huyo hakustahili kuchukuwa wadhifa huo kwa sababu kwa mtazamo wao, anaongoza bunge lisilo la kidemokrasia linalohodhiwa na chama kimoja.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW