Spitzenkandidaten: Mpambano wa nafasi za juu EU
28 Mei 2019Jean-Claude Juncker ndiye aliyekuwa wa kwanza kuteuliwa chini ya mchakato huo, ambao ulianzishwa mwaka 2014 katika jaribio la kuimarisha ushiriki wa wapigakura.
Chini ya mfumo huo, makundi ya kisiasa kutoka kote Umoja wa Ulaya huteua wagombea wake wa nafasi ya rais wa Halmashauri Kuu ya Ulaya, kwa ufahamu kwamba mgombea wa kundi au kambi inayopata matokeo mazuri zaidi katika uchaguzi wa bunge la Ulaya anapaswa kuwa wa kwanza kuzingatiwa kwa nafasi hiyo.
Hivyo wagombea wakuu, kwa Kijerumani, "Spitzenkandidaten" huipa sura kila kambi ya kisiasa ya Ulaya kwa wapigakura kujitambulisha nayo.
Watetezi wa mfumo huo wanasema hii inaufanya Umoja wa Ulaya kuwa na demokrasia na uwazi zaidi. Wakosoaji wanahoji hata hivyo, kwamba mfumo huo una kasoro nyingi kwa sababu makundi ya kisiasa ya Ulaya hayana orodha za kuvuka mataifa, hii ikimaanisha kuwa, mgombea yeyote mkuu anaweza tu kuteuliwa katika taifa lake.
Chini ya sheria ya Umoja wa Ulaya, rais wa Halmashauri Kuu anapaswa kuteuliwa kwanza na viongozi wakuu wa kitaifa wa kanda hiyo na kisha huhitaji wingi wa kura zisizopungua 376 katika bunge lenye jumla ya wabunge 751.
Kufuatia uchaguzi wa bunge la Ulaya uliofanyika wiki iliyopita, muungano wa makundi yasiyopungua matatu ya kisasa utahitajika kwa mgombea yeyote kupata kura zinazohitajika.
Chama cha European People's (EPP) kilishinda kura nyingi zaidi, hali inayomuweka mgombea wake - kiongozi wa kundi la wabunge, Manfred Weber, kutoka Ujerumani, katika nafasi ya usoni.
Kundi lililoshika nafasi ya pili la Wasoshalisti na Wanademokrasia pia wanajaribu kupata wingi kwa ajili ya mgombea wao, makamu wa rais wa halmashauri hiyo, Mholanzi, Frans Timmermans.
Kundi la Waliberali la ALDE, ambalo ndiyo la tatu kwa nguvu katika bunge jipya, linatumai kunufaika na migawanyiko miongoni mwa makundi mawili ya juu - na pia upinzani wa baadhi ya viongozi wa Umoja wa Ulaya dhidi ya mfumo wa "Spitzenkandidaten" kupata uungwaji mkono wa kutosha kwa mgombea wake, kamishna wa ushindani wa Umoja wa Ulaya Margrethe Vestager kutoka Denmark.
Hakuna wajibu wa kisheria hata hivyo kwa wabunge kufuata mfumo wa Spitzenkandidaten, na majadiliano magumu yanaweza kumaanisha kwamba mgombea wa nje anaweza kuwa mrithi ya Juncker.
(dpa)