1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UEFA yamuunga mkono Platini

16 Oktoba 2015

Kashfa ya hongo inayolikumba shirikisho la kambumbu la kimataifa FIFA ,kabumbu barani Afrika na Pistorius kutolewa jela mwaka mmoja baada ya kuhukumiwa kifungo cha miaka mitano kwa makosa ya kumuuwa mpenzi wake

Josef Blatter,mwenyekiti wa shirikisho la kabumbu la Ujerumani Wolfgang Niersbach(kulia) na mwenyekiti wa UEFA Michel Platini (Kati)Picha: picture-alliance/dpa/O. Weiken

Tuanzie lakini na kishindo cha kashfa ya hongo ya FIFA na jinsi kinavyotishia shughuli za shirikisho hilo.Kamati tendaji ya FIFA imepangiwa kukutana October 20 ijayo lakini suala la kuakhirishwa kuchaguliwa mwenyekiti mpya halimo katika ajenda ya mazungumzo.Haimaanishi lakini kwamba halitozushwa.

Hadi dakika hii tulio nayo,february 26 mwakani inasalia kuwa tarehe ya kuchaguliwa mwenyekiti mpya katika wakati ambapo vigogo viwili mashuhuri,Joseph Blatter aliyetangaza kujiuzulu kama mwenyekiti wa FIFA mhula wake utakapomalizika na Michel Platini, mwenyekiti wa UEFA , wamesitishiwa shughuli zao kwa muda wa siku 90 na kamati ya maadili ya FIFA.

Mbali na Platini,na mwanamfalme Ali wa Jordan,mwenyekiti wa shirikisho la kabumbu barani Asia pia Sheikh Salman Ben Ibrahim al Khalifa wa Bahrein wameshajitokeza kugombea wadhifa wa mwenyekiti wa shirikisho la kabumbu la kimataifa FIFA,uchaguzi utakapoitishwa february 26 ijayo kama hakuna mabadiliko yatakayotokea.

Tarehe ya mwisho ya kutuma maombi ni October 26 ijayo.Wengine wanaweza kujitokeza kugombea wadhifa huo,mfano wa mfungwa mwenza wa zamani wa Nelson Mandela, Tokyo Sexwale (SEKWALE),au Jerôme Champagne,aliyewahi kuwa naibu katibu mkuu wa shirikisho la kabumbu la kimataifa FIFA.

UEFA inaonyesha ina mpango mbadala

Mwenyekiti wa muda,Issa Hayatou wa Cameroun ameshakabidhiwa hatamu za uongozi tangu alkhamisi uiliyopita mjini Zurich,lakini mwenyewe ameshasema hatogombea wadhifa huo.

Suala kama mwenyekiti wa sasa wa shirikisho la vilabu vya dimba barani Ulaya UEFA,mfaransa Michel Platini ataweza kweli kugombea wadhifa huo bado halijapatiwa jibu.Alkhamisi iliyopita Platini alijipatia uungaji mkono "jumla "wa wanachama wa UEFA,ingawa hawakuondowa uwezekano,pindi ikilizamika kuwakilishwa na mgombea mwengine katika kinyang'anyiro cha kuania wadhifa wa mwenyekiti wa FIFA.

Katibu mkuu wa UEFA,GIANNI INFANTINO anasema:

"Nnafikiri,lolote litakalotokea mnamo siku chache zinazokuja,ingawa siamini hivyo,nafikiri tutakuwa tumeshafikia uamuzi wa mwisho hadi oktoba 26.Lakini nini kitatokea hadi wakati huo ni suala ambalo litajadiliwa na wawakilishi wa UEFA ndani ya FIFA pamoja na wanachama wa mashirikisho mengine,kama tulivyokuwa tukifanya zamani.Baadae tutaona kama kuna mtu mwengine atakaechomoza,kama kuna mtu mwengine kutoka shirikisho jengine atakaechomoza,kama ni mzungu au vipi...nahisi ni mapema mno kuashiria yote hayo."

Infantino amesisitiza UEFA wanaunga mkono haki ya Michel Platini ya kukabiliana na kesi ya haki na kupatiwa nafasi ya kujitakasa.Amezitolea wito taasisi zote husika,tume ya maadili ya FIFA,baraza linalopokea mashtaka la FIFa na korti inayosimamia masuala ya michezo zishikiane haraka kuhakikisha uamuzi kuhusu kadhia hii ya rushwa unafikiwa hadi ifikapo kati kati ya mwezi ujao wa Novemba.

Itafaa kusema hapa kwamba hata gwiji la soka ulimwenguni Pele wa Brazil amelalamika akisema yanayolikumba shirikisho la kabumbu FIFA ni aibu hata hivyo anasema anaamini kishindo hicho hakitachafua hadhi ya shirikisho hilo la dunia."Kabumbu bado ni mchezo wa kusisimua na hakuna yeyote anaeweza kuichafua sifa hiyo.

Mpira ni duwara

Hakukosea Pele aliposema dimba ni mchezo wa kusisimua...Na maajabu pia yanaweza kuzuka uwanjani.Kama ilivyoshuhudiwa jumanne iliyopita mjini Maseru nchini Lesotho pale timu ya visiwa vidogo vya Comoro katika bahari ya Hindi ilipozusha maajabu ya kuingia duru ya pili ya kuania tikiti ya kuingia katika fainali ya kombe la dunia nchini Urusi mwaka 2018-kanda ya Afrika.Maajabu kama hayo yamezushwa pia na Chad nchi nyengine isiyojulikana katika medani ya dimba barani Afrika.Les Coelacanthes au "Gombesa "kama timu ya taifa ya Comoros inavyoitwa,watafunga safari hadi Accra kupimana nguvu na watoto wa Black Stars wa Ghana waliowahi kuingia robo fainali katika michuano ya kombe la dunia mwaka 2010 nchini Afrika Kusini na kuinyemelea nafasi hiyo katika kombe la dunia mwaka 2014 nchini Brazil.Nimezungumza na ripota wetu wa Moroni Abubakar Oumar kutaka kujua matumaini ya gani wanajiwekea "Les Coelacanthes" kuelekea duru hizo za pili zitakazoanza Novemba 7 ijayo.Abubakar Oumar anasema wakomoro wanaamini maajabu yatatokea pia Accra.

Mbali na pambano kati ya Les Coelacanthes wa Comoro na Black Stars wa Ghana, michauno mengine ni pamoja na ule kati ya mabingwa watetezi wa Afrika Côte d'Ivoire dhidi ya Liberia,Algeria iliyoingia robo fainali katika kombe la dunia mwaka 2014 nchini Brazil itakayomenyana na Tanzania na Tchad itashindana na Misri.Tukiitaja kwa uchache.

Riadha

Shirikisho la riadha la Kenya-AK limeamua kuondowa marufuku yaliyowekewa taasisi mbili zinazowasimamia wanariadha mashuhuri wa mbio za marathon Dennis Kimetto na Wilson Kipsang.Volare Sports inayosimamiwa na Gerard van de Veen wa Uholanzi na lile la Rosa and Associati lenye makao yake nchini Italy zilifungiwa kwa muda wa miezi sita,April iliyopita kufuatia tuhuma dhidi ya wanariadha wa Kenya.Mwenyekiti wa shirikisho la wanariadha wa Kenya,Jackson Tuwei amesema taasisi zote hizo mbili zinaruhusiwa upya kuendesha shughuli zao ingawa uchunguzi unaendelea."Tumelazimika kupitisha uamuzi huu kwasababu sio wanariadha wote ni wakosa" -amesema Jackson Tuwei katika mkutano na waandishi habari.Zaidi ya hayo shirikisho la wanariadha wa Kenya linawachunguza mameneja wengine watatu baada ya zaidi ya wanariadha 30 wa Kenya kugunduliwa wametumia madawa marufuku ya kuimarisha misulimwaka 2012.Kwasasa wanariadha 15 wamezuwiliwa shughuli zapo kutokana na kadhia hiyo.Watatu kati yao wanasimamiwa na taasisi ya Rosa and Associati.

Na hatimae bingwa wa michezo ya Olympik ya walemavu,Oscar Pistorius wa Afrika kusini,inasemekana ataachiwa huru jumanne ya tarehe 20 octoba, ijayo,mwaka mmoja tangu alipoanza kutumikia kifungo cha miaka mitano jela kwa makosa ya kumuuwa mpenzi wake Reeva Steenkamp.

Habari hizo zilipotangazwa baadhi ya watu walishangiria katika barabara za mji mkuu Pretoria.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/SID/

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW