1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Sri Lanka inawezaje kusalimika na kuporomoka kwa uchumi?

21 Julai 2022

Msaada kutoka IMF utakuwa muhimu katika kuleta utulivu wa kifedha wa Sri Lanka, lakini wakosoaji wanasema kisiwa hicho kinahitaji kukabiliana kwanza na uhaba wa chakula na ukosefu wa utulivu wa kisiasa.

Sri Lanka's Prime Minister Ranil Wickremesinghe
Picha: Adnan Abidi/REUTERS

Rais mpya wa Sri Lanka Ranil Wickremesinghe ambaye amechaguliwa na bunge jana Jumatano, atakuwa na kazi kubwa ya kuikwamua nchi hiyo kutoka katika mzozo wake wa kiuchumi. Uchumi wa kisiwa hicho cha Bahari ya Hindi uliolemewa na madeni uliporomoka baada ya kukosa fedha za kulipia chakula, mafuta na dawa, na hivyo kuzua maandamano yaliyodumu kwa miezi kadhaa.

Serikali ya Sri Lanka inadaiwa dola za Marekani bilioni 51 ambazo inatatizika kulipa pamoja na riba ya mkopo wenyewe. Wachambuzi wengi wamelaumu miaka mingi ya usimamizi mbaya na ufisadi kuwa ndio chanzo cha matatizo hayo, ikiwa ni pamoja na kuchukua mikopo kizembe kutoka China, ambayo ilitumika kufadhili miradi kabambe ya miundombinu iliyogeuka kuwa mzigo kwa uchumi wa Sri Lanka.

Mgogoro wa madeni ulizidishwa na sera mbovu, ikijumuisha kupunguzwa kwa ushuru miezi michache kabla ya janga la COVID-19, mabadiliko ya ghafla katika sekta ya kilimo yaliyosababisha kupungua kwa mazao.

Miongoni mwa mambo mengine yaliyopelekea mambo kuwa mabaya zaidi ni kupungua kwa mapato ya watalii ambayo ndiyo chanzo muhimu cha upatikanaji wa fedha za kigeni. Na hii ni kufuatia mashambulizi ya kigaidi kipindi cha sikukuu ya Pasaka mwaka 2019.

Uchumi wa Sri Lanka unaelekea kudorora hadi kufikia asilimia 8 mwaka huu, wakati gharama za bidhaa nyingi kama chakula na mafuta zikiwa zimeongezeka mara tatu huku sarafu ya nchi hiyo ikiporomoka kwa asilimia 80.

Picha: ANDREW CABALLERO-REYNOLDS/AFP

Je, dhamana ya IMF inaweza kupatikana?

Kipaumbele cha kwanza kwa serikali mpya kitakuwa kusawazisha madeni makubwa ya Sri Lanka. Mazungumzo ya kupata msaada kutoka kwa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) tayari yanaendelea lakini yatahitaji marekebisho zaidi ya mikopo iliyopo ya IMF pamoja na ile ya China, India na Japan.

Kuna uwezekano msaada wowote ukaambatana na masharti, ikiwa ni pamoja na ubinafsishaji wa makampuni yanayomilikiwa na serikali na hatua kali zaidi za kiuchumi.

Ahilan Kadirgamar, mwanauchumi wa kisiasa katika Chuo Kikuu cha Jaffna, ameiambia DW kuwa raia hawana uwezo wa kuhimili hatua kali zaidi za kiuchumi, akiongeza kuwa karibu theluthi mbili ya watu wa Sri Lanka wanafanya kazi katika uchumi usio rasmi.

Kadirgamar ana mashaka juu ya msaada wa IMF akisema Colombo itapata tabu kuongeza deni lake la nje kwani gharama itakuwa kubwa mno kwa nchi ambayo tayari imeshindwa kulipa madeni yake.

Msaada zaidi unahitajika ili 'kuepusha baa la njaa'

Kadirgamar ametoa wito kwa rais mpya kutumia mapato ya fedha za kigeni ya Sri Lanka ambayo amesema yamefikia dola bilioni 1.3 hadi dola bilioni 1.5 kwa mwezi, ili kutoa kipaumbele katika uagizaji wa bidhaa muhimu kama vile chakula, mafuta na dawa ambavyo bado havijapatikana. Serikali lazima pia iongeze matumizi ya nakisi ili kufadhili misaada zaidi kwa umma, huku tishio la njaa likiongezeka.

Serikali ya awali ya Rais Gotabaya Rajapaksa, ambaye alikimbilia Singapore na kujiuzulu akiwa uhamishoni,  tayari imebatilisha baadhi ya makosa ya kisera yaliyochochea mgogoro huo. Lakini wengi wao wanaweza kuchukua miaka kadhaa kuisaidia nchi hiyo kupata ahueni.

Hatua ya kupunguzwa kwa ushuru yaondolewa

Kwa mfano, hatua za punguzo kubwa la ushuru iliyotangazwa mnamo mwaka 2019 ili kuchochea ukuaji wa kiuchumi ilifutwa mwezi uliopita ili angalau kukidhi masharti ya msaada uliopendekezwa na shirika la IMF. Kulingana na kituo cha habari cha Bloomberg, uamuzi huo wa awali ulipelekea kushuka kwa mapato kwa kiasi cha rupia bilioni 800 ambazo ni sawa na dola bilioni 2.2 kwa mwaka.

Marekebisho hayo yanamaanisha kuwa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) na kodi za mashirika zinapandishwa kwa wakati mbaya zaidi na huenda zikashindwa kuongeza mapato ya kutosha ya kodi huku uchumi wa taifa hilo ukiwa katika wakati mbaya zaidi.

Picha: Raminder Pal Singh/AA/picture alliance

Kuchochea kilimo baada ya mazao kuharibika

Mnamo Novemba, serikali pia ilifanya majaribio makubwa ya kilimo, miezi michache tu baada ya kutangaza marufuku ya nchi nzima kwa matumizi ya mbolea na viuatilifu. Matokeo yake, uzalishaji wa ndani wa mchele ulipungua kwa theluthi moja huku uzalishaji wa majani chai ambayo ndio chanzo kikuu cha fedha za kigeni, ulipungua kwa asilimia 16.

Utalii, pia, unaweza kuchukua muda mrefu kurejea katika hali yake ya kawaida. Mapato yatokanayo na watalii nchini Sri Lanka yalifikia dola bilioni 4.3 mwaka 2018 lakini yalipungua karibu kwa asilimia 80 wakati wa janga la ugonjwa wa COVID19.

Wakati nchi nyingi za Asia zikishuhudia hivi karibuni ongezeko la watalii, vurugu za wananchi zilizoenea na usumbufu mkubwa uliopo Sri Lanka vimewafurusha watalii walio wengi.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW