1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Sri Lanka yatangaza hali ya dharura baada ya rais kukimbia

13 Julai 2022

Sri Lanka imetangaza hali ya dharura baada ya Rais Rajapaksa na mke wake kukimbilia nchini Maldives, saa chache kabla ya kufika kwa muda wake wa kuachia ngazi. Waziri Mkuu Ranil Wickremesinghe amekuwa kaimu rais.

Sri Lanka Colombo | Proteste am Büro des Premierministers Ranil Wickremesinghe
Picha: Adnan Abidi/REUTERS

Saa kadhaa baada ya Rais Gotabya Rajapaksa kuikimbia Sri Lanka mapema leo, ofisi ya waziri ilitagaza hali ya dharura. Licha ya kutangazwa hatua hiyo maelfu ya waandamanaji waliendelea kumiminika katika ofisi ya waziri mkuu Ranil Wickremesinghe, ambaye hivi sasa ndiye kaimu rais, wakimtaka ajiuzulu, huku polisi ikijibu kwa kufyetua gesi ya kutoa machozi.

Msemaji wa waziri mkuu Dinouk Colombage amesema waziri mkuu kama kaimu rais ametangaza hali ya dharura kote nchini humo na kuweka marufuku ya kutembea usiku katika mkoa wa magharibi.

Soma pia: Rais Rajapaksa wa Sri Lanka huenda akakimbia nchi

Mapema leo, afisa wa uhamiaji alisema rais na mke wake, pamoja na walinzi wawili, waliondoka nchini humo kwa ndege ya jeshi la Sri Lanka. Chanzo kutoka serikalini kimesema ndege hiyo ilitua katika mji mkuu wa Maldives, Male, na baadaye kuthibitishwa na jeshi la anga la Sri Lanka.

Utorokaji huo wa mapema wa rais unafuatia maandamano makubwa katika taifa hilo, ambalo limekuwa likikabiliana na mzozo mbaya wa kiuchumi, yaliyofikia kilele kwa uvamizi wa makaazi rasmi ya rais na waziri mkuu siku ya Jumamosi.

Waandamanaji wakiwa wamekusanyika mbele ya ofisi ya waziri mkuu wa Sri Lanka mjini Colombo, wakimshinikiza kujiuzulu, Julai 13, 2022.Picha: Adnan Abidi/REUTERS

Mapambano yanaendelea

Uonyeshaji huo wa ghadhabu za umma ulimlazimisha Rajapaksa kwenda mafichoni na kumpelekea kukubali kuachia madaraka leo Jumatano, hivyo kusafisha njia ya makabidhiano ya amani ya madaraka.

Hata hivyo Rajapksa anakabiliwa na mashtaka kadhaa ya uhalifu na inaaminika aliondoka nchini humo kabla ya kujiuzulu na kupoteza kinga yake ya urais.

Soma pia: Sri Lanka bado yakabiliwa na mkwamo wa kisiasa

Hata hivyo mwanaharakati Chintaka Pradeep anasema kukimbia hakutomsaidia Rajapaksa. "Hakukuwa na njia kwa rais kusalia nchini. Amekuwa mafichoni wakati wote huu hivyo atalazimika kuishi nje ya nchi."

"Lakini kwa sababu tu ameondoka haimaanishi mapambano yameisha. Kama amepora, basi mapambano yataendelea hadi kila kitu kikamatwe. Kama waandamanaji, tunachosema ni kwamba hawezi kukwepa kwa sababu tu ameondoka nchini," alisema Pradeep.

Uchaguzi Julai 20

Kabla ya kukimbia, Rais Rajapaksa alimteuwa waziri mkuu kuwa kaimu rais kulingana na muongozo wa katiba. Waziri mkuu Wickremesinghe pia atajiuzulu endapo muafaka utafikiwa juu ya kuundwa kwa serikali ya umoja.

Upo uwezekano kwamba spika wa bunge, Mahinda Yapa Abeywardena, atachukuwa uongozi wa nchi hadi rais mpya atakapochaguliwa, katika kura itakayofanyika Julai 20.

Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani, Sajith Premadasa, aliyeshindwa na Rajapaksa katika uchaguzi wa rais wa mwaka 2019, amesema atawania nafasi hiyo.

Baadhi ya wanachama wa chama tawala cha sasa pia wametoa wazo la Wickremesinghe kuwania nafasi ya rais. Lakini wanaharakati wa maandamano wamesema hawatomtambua kama rais hata akigombea.

Chanzo: dpa, ap, afp, Reuters

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW