1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Steinmeier achaguliwa rais wa Ujerumani kwa muhula wa pili

13 Februari 2022

Wanasiasa wa Ujerumani na wajumbe kutoka kote nchini Ujerumani wamemchagua tena Frank-Walter Steinmeier kushika nafasi ya mkuu wa nchi, ambayo kwa sehemu kubwa ni ya heshima tu.

Deutschland | Bundesversammlung | Bundespräsident Steinmeier wiedergewählt
Picha: Michael Probst/AP Photo/picture alliance

Frank-Walter Steinmeier amechaguliwa kwa muhula wa pili kama rais wa Ujerumani siku ya Jumapili.

Rais huyo ambaye alikuwa akitetea nafasi yake aliungwa mkono na asilimia 77 ya Bundesversammlung (Mkutano Maalumu wa Shirikisho) mjini Berlin.

Mkutano huo ulihusisha wabunge wa bunge la Ujerumani Bundestag, au Baraza la chini la bunge, pamoja na idadi sawa ya wajumbe waliochaguliwa na majimbo 16 yanayounda taifa hilo.

Nini alichokisema Steinmeier baada ya kuchaguliwa tena?

Katika hotuba yake ya kukubali muhula wa pili wa miaka mitano, Steinmeier alisema yupo upande wa kila moja anaetetea demokrasia na alionya juu uwezekano wa vita endapo Urusi itaivamia Ukraine.

Rais Steinmeier akipokea maua kutoka kwa wajumbe wa mkutano maalumu uliomchagua kwa muhula wa pili wa miaka mitano, Februari 13, 2022.Picha: Michael Probst/AP Photo/picture alliance

"Tuko katikati mwa hatari ya mzozo wa kijeshi, vita mashariki mwa Ulaya," alisema Steinmeier katika mkutano maalumu, na kuongeza kuwa "Urusi inabeba dhamana ya hili.

Soma pia: Rais Steinmeier aungwa mkono na chama kikuu cha upinzani

"Namuomba rais (wa Urusi) Putin: Legeza kamba kwenye shingo ya Ukraine na utafute pamoja nasi njia inayotunza amani barani Ulaya," alisema.

Steinmeier pia alikataa kuepuka makabiliano na wapinzani wenye msimamo mkali dhidi ya hatua za serikali za kupambana na maradhi ya Covid-19, akimaanisha vuguvugu la Querdenker ambalo linaeneza uongo na dhana za njama.

"Kwa wale wanaochana madonda yalio wazi, wanaoeneza chuki na uongo katika dhiki ya janga, wanaozungumza juu ya 'udikteta wa Corona' na wanaotoa vitisho na kufanya vurugu dhidi ya askari polisi wa kike, wauguzi na mameya, kwao nasema: 'Niko hapa, Nabaki," alisema rais.

Lakini pia alikiri kwamba janga "limesababisha madonda makubwa katika jamii yetu" na makosa yamefanyika. "Lakini, mabibi na mabwana, nionesheni mfumo wa kiimla ambao ungepita katika mzozo huu kwa namna iliyo bora zaidi."

Mafanikio makubwa katika mapambano dhidi ya COVID yalikuwa utengenezaji wa haraka wa chanjo na Ujerumani pamoja na washirika barani Ulaya na Marekani, Steinmeier alisema.

Steinmeier akipongezwa na mke wake Elke Buedenbender.Picha: MICHAEL SOHN/POOL/AFP via Getty Images

"Kwa ukosoaji wote wa nafsi unaohitajika, hatupaswi kuficha uwezo wetu."

Ni nani walikuwa wagombea?

Rais Steinmeier, 66, mwanachama wa chama cha Social Democratic, SPD, ambaye alihudumu mihula miwili kama waziri wa mambo ya nje wa kansela wa zamani Angela Merkel na hapo kabla alikuwa mkuu wa ofisi ya kansela wa zamani Gerhard Schröder, anapendwa sana miongoni mwa umma wa Wajerumani.

Soma pia: Steinmeier ahimiza mshikamano kwa wajerumani

Uchunguzi wa karibuni wa maoni ya wananchi ulionesha kuwa asilimia 85 ya Wajerumani wanaamini alikuwa anafanya kazi nzuri, na anafurahia uungaji mkono wa muungano tawala na vyama vikuu vya upinzani vya kihafidhina.

Wagombea wengine watatu walikuwa mwanasiasa wa mrengo wa kushoto Gerhard Trabert, 65, aliegombea kupitia chama cha mrengo wa kushoto, mwanafizikia Stefanie Gebauer, 41, ambaye aliteuliwa na kundi la kisiasa linalojulikana kama Free Voters, na Max otte, 57, mchumi mhafidhina aliechaguliwa na chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha Alternative for Germany (Chama Mbadala kwa Ujerumani), AfD.

Steinmeier akihutubia mkutano maalumu baada ya kuchaguliwa.Picha: Michele Tantussi/REUTERS

Mgombea wa mwisho alizusha mjadala kwenye nyanja ya kisiasa nchini Ujerumani, kwa sababu Otte siyo mwanachama wa AfD na anasalia kuwa sehemu ya chama kikuu cha cha Christian Democratic Union (CDU). Viongozi wa CDU wameapa kufuta uanachama wake.

Upigaji kura ulifanyikaje?

Mkutano Maalumu wa shirikisho haukufanyika katika majengo ya Reichtag kama ilivyo ada, kutokana na  sheria za janga zinazohitaji wapigakura kukaa mita 1.5 (futi 5) mbalimbali.

Soma pia: Steinmeier: Kushindwa kwa utawala wa Manazi ni ukombozi

Badala yake, kura ilifanyika katika jumba jirani la Paul Löbe, ambapo wajumbe walisambazwa katika vyumba kadhaa na maghorofa. Kura hiyo ilikuwa ya siri, ambapo wajumbe waliitwa majina yao kwenye vibanda kwa kufuata utaratibu wa alfabeti.

Kati ya jumla ya kura 1,437, Steinmeier alipata kura 1045. Otte alipata kura 140, Trabet alipata 96,  na Gebauer alipata kura 58. Kulikuwa na wajumbe 86 ambao hawakuwepo na kura 12 ziliharibika.

Rais wa Ujerumani hufanya nini?

Wakati marais wa Ujerumani huwa na mamlaka kidogo ya kiutendaji, wanalenga kuwa mamlaka ya kimaadili juu ya siasa za kila siku.

Mtu anaeshikilia wadhifa huo anasaini miswada kuwa sheria na kuiwakilisha Ujerumani kwenye hafla mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Wakati wa muhula wa kwanza wa Steinmeier madarakani, alikuwa kinara wa demokrasia ya kiliberali nchini Ujerumani na nje, na alihimiza mjadala kuhusu masuala nyeti hivi karibuni, ambayo yalijumuisha mipango ya chanjo ya laazima dhidi ya virui vya corona.

Chanzo: DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW