1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Steinmeier ahimiza ushirikiano wa kimataifa

Sekione Kitojo
21 Novemba 2018

Rais wa Afrika kusini Cyril Ramaphosa amesema Ujerumani ni mshirika muhimu wa kiuchumi wa nchi hiyo ambapo alionesha matumaini  juu ya ushirikiano huo kupanua fursa za uwekezaji wa Ujerumani katika nchi yake.

Bundespräsident Steinmeier in Südafrika
Picha: picture-alliance/dpa/B. von Jutrczenka

Cyril Ramaphosa ameyasema  hayo  jana (20.11.2018)mjini  Cape Town  wakati  rais  wa  Ujerumani Frank-Walter  Steinmeier akimaliza  ziara  yake  ya  siku  tatu  nchini  humo. 

Ramaphosa  alisema  Ujerumani  ni mshirika  mkubwa  wa  tatu  duniani wa  kibiashara   wa  Afrika  kusini   na  ni  mmoja  kati  ya  wawekezaji wakubwa  wa  kigeni  katika  nchi  hiyo. Amesema  zaidi  ya  makampuni 600  ya  Ujerumani  yanafanyakazi  nchini  Afrika  kusini, ambapo yameweza  kutengeneza  nafasi  zaidi  ya  laki  moja  za  kazi.

Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier (kushoto) na rais wa Afrika kusini Cyril Ramaphosa ( kulia )Picha: picture-alliance/dpa/B. von Jutrczenka

"Kama  ilivyoonekana  katika  mazungumzo yetu  na  viongozi  wa makampuni  ya  Ujerumani  mjini  Berlin mwezi  uliopita, Afrika  kusini inaonekana  kuwa  sehemu  muhimu  ya  uwekezaji. Na  kuna  hamasa kubwa  kwa  makampuni  ya  Ujerumani  kupanua uwapo  wao hapa."

Ujerumani  na  Afrika  kusini  zitakuwa  wanachama  ambao  si  wa kudumu  katika  baraza  la  Usalama  la  Umoja  wa  Mataifa  kwa mwaka  2019  na  2020   na  rais  Cyril Ramaphosa  amesema wamekubaliana  kwamba  nchi  zao  zitafanyakazi  kwa  pamoja kuhimiza  amani  ya  dunia   na  usalama  pamoja  na  kuimarisha mfumo  wa  ushirikiano  wa  pamoja.

Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier akilakiwa kwa gwaride la kijeshi nchini Afrika kusiniPicha: picture-alliance/dpa/B. von Jutrczenka

Siasa za kizalendo

Rais  wa  Ujerumani Frank-Walter Steinmeier  alionya  kuhusu siasa  za  kizalendo , na  kutoa  wito  wa ushirikiano  zaidi  kimataifa.

"Nafikiri kumekuja  wakati  ambao  utaratibu wa  kimataifa  umekabiliwa na  mbinyo. wanaopendelea  ushirikiano  wa  pamoja  na  wanapendelea utaratibu huu kuendelea  na  kuulinda. Ni  muhimu kuangalia  matumaini hayo  na  kufanyakazi kwa  pamoja   katika  baraza  la  Usalama  la Umoja  wa  mataifa."

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New YorkPicha: picture-alliance/Xinhua News Agency/L. Muzi

Dunia  haitakuwa  na  amani  kwa  mtazamo  wa  kila  mmoja  dhidi  ya kila  mwingine, lakini  kwa  kutumia  ushirikiano  zaidi,  amesema Steinmeier. Kwa  bahati  mbaya, si  kila  mmoja  analiangalia  suala hilo  kwa  njia  hiyo, ameongeza, bila  ya  kumtaja  rais  wa  marekani Donald  Trump ama  kiongozi  mwingine  wa  serikali.

Akiongozana  na ujumbe  wa  ngazi  ya  juu  wa  viongozi  wa  makampuni, Steinmeier, ambaye  ziara  yake  imelenga  katika  kuimarisha  mahusiano  baina ya  mataifa  hayo  mawili, alikutana mjini  Johannesburg  na  wawakilishi wa  sekta ya  biashara  na  vyama  vya  kijamii.

Mwandishi: Kroll, Katharina / ZR /  Sekione  Kitojo

Mhariri: Idd Ssessanga

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW