1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Steinmeier aitaka Iran ifikia muafaka wa nyuklia

12 Machi 2015

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier ameitaka Iran kuonyesha kwamba iko tayari kufikia muafaka wakati mazungumzo juu ya mpango wake wa nyuklia wiki ijayo.

Waziri wa Mambo ya nje wa Ujerumani Frank Walter (kushoto) akimpa mkono waziri wa Mambo ya nje wa Marekani John Kerry baada ya kuzungumza na waandishi wa habari Washington(11.03.2015)
Waziri wa Mambo ya nje wa Ujerumani Frank Walter (kushoto) akimpa mkono waziri wa Mambo ya nje wa Marekani John Kerry baada ya kuzungumza na waandishi wa habari Washington(11.03.2015)Picha: picture-alliance/dpa

Waziri huyo wa mambo ya nje wa Ujerumani amesema ni wazi kwamba kile wanachokitaka kukiona ni kwamba linakuwa jambo lisilowezekana kwa Iran kuwa na bomu la nyuklia.

Amesema"Nigelipenda kusema kwa mara nyengine tena hili sio suala la kuchanganuwa baina ya kuwa na makubaliano mazuri au mabaya. Ujumbe wetu uko wazi fursa kwa Iran kutengeneza bomu la nyuklia lazima itokomezwe lazima iyakinishwe hivyo kwa muda mrefu.Tunahitaji kuwa na usalama zaidi na sio usalama mdogo.Na kigezo hiki kitatumika katika kila juhudi za kupata ufumbuzi wa mzozo huo."

Steinmeir akizungumza na waandishi wa habari kufuatia mkutano wake na waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry mjini Washington hapo Jumatano wakati wa awamu muhimu ya mazungumzo ya nyuklia na Iran na mzozo wa Ukraine.

Steinmeir amesema kumekuwepo na maendeleo katika mazungumzo wakati wa duru ya mwisho ya mazungumzo hayo ya nyuklia lakini amesema yeye na waziri mwenzake Kerry wana maoni yanayolingana kwamba sio vikwazo vyote vimeweza kupatiwa ufumbuzi katika mazungumzo hayo na ameitaka Iran kuonyesha kwamba inachukuwa hatua kuupatia ufumbuzi wa mzozo wake huo wa nyuklia.

Maamuzi ya msingi yanahitajika

Katika mkutano huo wa pamoja na waandishi wa habari Kerry amesema Iran inatakiwa kufanya maamuzi ya msingi kuithibitishia jumuiya ya kimataifa kwamba haitaki kutengeneza silaha za nyuklia.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani John Kerry.Picha: Mark Wilson/Getty Images

Kerry amekaririwa akisema "Ni muhimu sana kwamba Iran inafanya maamuzi ya msingi kama tunavyofanya sisi ili kujaribu kuithibitishia dunia kadri inayvowezekana kwamba hakutakuwepo na fursa ya kutengeneza silaha za nyuklia na kwamba dunia inaweza kuwa na uhakika na shughuli za Iran."

Waziri wa mambo ya nje wa Iran Mohammed Javad Zarif hapo Jumatatu atakuwa na mazungummzo mjini Brussels na mawaziri wenzake kutoka Ujerumani,Ufaransa na Uingereza kama sehemu ya juhudi za kufikia makubaliano.Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini atakuwa mwenyeji wa mkutano huo.

Uaminifu wa Marekani mashakani

Hapo Jumatano waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry alishutumu baruwa iliyotumwa nchini Iran na maseneta wa chama cha Republican yenye kupinga mazungumzo hayo anayoyaongoza kwa kusema kwamba inahatarisha uaminifu wa dunia kwa Marekani.

Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani (kushoto) na waziri wa Mambo ya nje wa Iran Mohammad Javad Zarif.Picha: Reuters/E. Vucci

Mawaziri wa mambo ya nje wa Ujerumani na Marekani katika mazungumzo yao mjini Washington pia wamegusia suala la mzozo wa Ukraine na kusisitiza kuheshimiwa kwa makubaliano ya amani ya Minsk na pande zote mbili zilioko kwenye mzozo huo na pia kuondowa silaha nzito kwenye eneo la mapigano.

Mawaziri hao hapo pia wamesema kwamba ni muhimu kwa Urusi kuacha kuunga mkono ukiukaji wa uhuru wa Ukraine na haki yake ya kujitawala.Wamesema ni muhimu kutekelezwa kwa makubaliano ya Minsk ili kuhakisha Ulaya inabakia kuwa huru,kitu kimona na ina amani.

Mwandishi:Mohammed Dahman /dpa/AFP

Mhariri:Yusuf Saumu

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW