Steinmeier aonya kuhusu mkataba wa Iran
7 Mei 2018Rais wa Shirikisho la jamhuri ya Ujerumani Frank-Walter Steinmeier ameeleza wasiwasi wake kuhusu kuibuka kwa vita iwapo mkataba wa nyuklia wa Iran utavunjika, huku akiwasifu viongozi wa Ulaya kwa kuliibua suala hilo katika ziara zao nchini Marekani. Aidha, Steinmeier ameelezea pia hofu yake kuhusu mabadiliko makubwa ya kimahusiano kati ya mataifa ya Ulaya na Marekani, wakati kukiwa na mvutano mkubwa miongoni mwao kuhusiana na masuala ya biashara, ulinzi na mkataba wa nyuklia.
Steinmeier alikuwa akizungumza katika mahojiano na kituo cha utangazaji cha Ujerumani- ARD alimnukuu waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry aliposema "pengine tumevizuia vita" wakati mataifa saba yaliposaini mkataba huo wa nyuklia mwaka 2015. Steinmeier amesema nukuu hiyo ni muhimu kwa kuwa kila mmoja atalazimika kufikiria kile kinachoweza kutokea iwapo mkataba huo utavunjika, na hatimaye Mashariki ya Kati kuanza kujiimarisha kisilaha.
Rais Donald Trump wa Marekani amekuwa akitishia kujiondoa kwenye mkataba huo, uliofikiwa mwaka 2015 kati ya Iran na mataifa sita yenye nguvu zaidi kiuchumi ambayo ni pamoja na Ufaransa na Ujerumani. Mei 12 ambayo ni tarehe ya mwisho iliyowekwa na Trump inakaribia, na anatarajiwa kutoa maamuzi rasmi ya iwapo ataendelea kuunga mkono mkataba huo ama la.
Lakini pia kwenye mahojiano hayo, Steinmeier amezungumzia wasiwasi kuhusu kuibuka kwa visa vya ubaguzi dhidi ya Wayahudi nchini Ujerumani, akionya havitakiwi kuvumiliwa, na vinaweza kuondoa hisia ya watu kujisikia wapo nyumbani hususan kwa wale wanaotaka kuishi nchini hapa.
Alisema na hapa namnukuu, "awe Myahudi, Mkristo au Muislamu, awe ni muumini au asiyeamini, wawe wameishi hapa kwa muda mrefu ama la, watu wanataka kujihisi wapo nyumbani wanapokuwa Ujerumani" mwisho wa kumnukuu.
Steinmeier ametaja hofu yake kuhusu mabadiliko makubwa ya mahusiano kati ya mataifa ya Ulaya na Marekani, katika wakati ambapo kuna mvutano mkubwa kati ya mataifa hayo na rais Donald Trump wa juu ya masuala ya biashara, ulinzi na mkataba wa nyuklia wa Iran.
Amekiri kwamba Ujerumani ambayo ni taifa lenye nguvu zaidi kiuchumi barani Ulaya, ambalo kwa muda mrefu limekuwa likifaidika na ulinzi wa Marekani chini ya mwamvuli wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO, hivi sasa linapaswa kujiimarisha na kutambua majukumu yake ya kimataifa.
Steinmeier alinukuliwa akisifu ziara zilizofanywa na viongozi wa Ulaya nchini Marekani mwezi uliopita, ambapo rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron na kansela wa Ujerumani Angela Merkel walizungumzia maslahi ya Ulaya na uendelezwaji wa mkataba huo, pamoja na masuala ya biashara.
Aidha Steinmeier ameonya dhidi ya kuongezeka kwa hatua za mataifa ya magharibi ya kumtenga rais wa Urusi, Vladimir Putin, akisema kwamba hata kama Urusi ilikuwa ikijipambanua yenyewe kwa kujitofautisha na Ulaya badala ya kushirikiana, diplomasia ni lazima iwe mkakati na fursa mpya yakuwa na mazungumzo.
Mwandishi: Lilian Mtono/DPAE/AFPE.
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman