1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Steinmeier asema hali Mashariki mwa Ukraine hairidhishi

Mjahida 10 Novemba 2014

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier amesema hali katika maeneo yanayoshikiliwa na waasi, Ukraine imeanza tena kuwa tete na pande zote zinapaswa kuheshimu makubaliano ya kusitisha mapigano.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Frank-Walter SteinmeierPicha: picture-alliance/dpa/Thomas Imo

Tamko la Waziri Frank-Walter Steinmeier alilolitoa wakati akiwa ziarani nchini Kazakhstan, lilionesha wasiwasi wake kufuatia ongezeko la mapigano mjini Donetsk na Luhansk kati ya vikosi vya serikali na waasi wanaotaka kujitenga wanaoiunga mkono Urusi.

Hali hii imetoakea licha ya kuwepo makubaliano ya kusitisha mapigano yaliotiwa saini katika mji mkuu wa Belarus, Minsk tarehe tano Septemba.

"Kwa bahati mbaya, hali imerejea tena kuwa tete sasa nafikiri tunapaswa kuwaita wale wote wanaousika na mgogoro huu, pamoja na upande wa Urusi kurejea kuangalia tena makubaliano ya Minsk," alisema Steinmeier katika mkutano na waandishi habari.

Waziri huyo wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani ameongeza kuwa atakaporejea mjini Berlin hii leo jioni atajadili hali ya Ukraine na Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini.

Baadhi ya wanajeshi wa Mashariki mwa UkrainePicha: picture-alliance/dpa

Aidha eneo la Donetsk Mashariki mwa Ukraine lilishuhudia mapigano makali siku ya Jumapili huku shirika la Usalama na Ushirikiano la Ulaya OSCE likisema limeona magari ya kijeshi yasiokuwa na nembo yoyote, katika maeneo ya waasi ambapo Ukraine kupitia msemaji wa baraza la usalama wa Kitaifa Andriy Lysenko, inaamini kuwa Urusi ndio iliyotuma jeshi lake huko.

"Katika eneo la Makiivka mjini Donetsk unaodhibitiwa na waasi kulionekana msururu wa magari 40, baadhi yao yakiwa na silaha nzito, Hasa makombora. Pia waangalizi wa shirika la usalama na ushirikiano la Ulaya waliwaona wanajeshi waliovalia sare ya kijivu bila ya utambulisho wowote," alisema Andriy Lysenko.

Waathiriwa wa ajali ya ndege ya Malaysia MH17 wakumbukwa

Kwa sasa pande zote mbili, serikali ya Ukraine na waasi, wanalaumiana kwa kukiuka mpango wa amani. Kwa upande wake Urusi imekataa kuwa inachochea mzozo wa Ukraine ikisema haijatuma wanajeshi au silaha Mashariki mwa Ukraine.

Wakati huo huo Uholanzi hii leo imeandaa ghafla ya Kitaifa ya kuwakumbuka waathiriwa waliopoteza maisha katika ajali ya ndege ya Malaysia MH17, ilioanguka Mashariki mwa Ukraine Julai 17.

Kumbukumbu ya waathiriwa wa ajali ya ndege ya Malaysia ya MH17Picha: Getty Images/J. Juinen

Rais wa Urusi Vladimir Putin amemuambia Waziri Mkuu wa Malaysia Najib Abdul Razak katika mkutano wa Viongozi mjini Beijing kwamba kuendelea na uchunguzi katika eneo la Mashariki mwa Ukraine palipoanguka ndege hiyo, imekuwa hatari kwasababu wanajeshi wa serikali ya Ukraine wameendelea kushambulia eneo hilo.

Hata hivyo Ukraine imekuwa ikiwalaumu waasi wanaotaka kujitenga kusababisha ajali hiyo ya ndege ambapo watu wote 298 waliuwawa. Urusi nayo imesema Ukraine inapaswa kulaumiwa kwa kuwa ingefaa iwajibike katika eneo lake la anga.

Mwandishi: Amina Abubakar/Reuters/dpa

Mhariri: Mohammed Abdul-rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW